OWM YATOA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI WA SHAHADA YA USIMAMIZI WA HATARI ZA MAAFA KUTOKA UDOM
KATIKA kuendelea kuimarika kwa sekta ya usimamizi wa maafa nchini na kuongezeka kwa hamasa ya kujifunza mifumo ya usimamizi wa maafa, tahadhari ya mapema na uratibu wa dharura, wanafunzi wa Shahada ya Usimamizi wa Hatari za Maafa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wamefanya ziara ya mafunzo kupitia Idara ya Usimamizi wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).
Ziara hiyo imefanyika tarehe 10 na 11 Juni, 2026 iliyolenga kuwajengea uelewa kwa vitendo kuhusu mifumo ya usimamizi wa maafa, ufuatiliaji wa vihatarishi mbalimbali, utoaji wa taarifa za tahadhari ya mapema pamoja na uratibu wa operesheni za dharura nchini.
Katika ziara hiyo, wanafunzi walitembelea Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichopo Ngome, Chumba cha Ufuatiliaji wa Mienendo ya Majanga na Tahadhari za Mapema kilichopo Mtumba pamoja na eneo la ujenzi wa Kituo Kikuu cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa na Maghala ya Kuhifadhi Vifaa vya Dharura kilichopo Nzughuni, jijini Dodoma.
Akizungumza na wanafunzi hao, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi, aliwapongeza kwa uamuzi wao wa kujifunza kwa vitendo kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa na kuonesha dhamira ya kuchangia maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Dkt. Yonazi aliwahimiza wanafunzi kuendelea kujiongezea maarifa kupitia tafiti, ubunifu na uandishi wa machapisho mbalimbali kuhusu usimamizi wa hatari za maafa ili kuchangia katika kuimarisha uwezo wa Taifa wa kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa.
Aidha, aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu ya juu katika kukuza taaluma ya usimamizi wa maafa na kuahidi kutembelea Chuo Kikuu cha Dodoma siku zijazo kwa ajili ya kutoa mihadhara na kushiriki katika mijadala ya kitaaluma.
“Ziara yenu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na Serikali katika kujenga kizazi cha wataalamu wenye uelewa wa kina kuhusu usimamizi wa hatari za maafa, tahadhari ya mapema na uratibu wa dharura. Aidha, inaonesha mafanikio ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa maafa, jambo ambalo limeendelea kuvutia wadau mbalimbali, watafiti na wanafunzi kutoka ndani na nje ya nchi kujifunza na kubadilishana uzoefu,”alisema Dkt. Yonazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maafa, Brigedia Jenerali Hosea Ndagala, aliwaeleza wanafunzi hao kuwa wamefanya jambo la msingi kwa kutenga muda wa kujifunza na kushuhudia kwa vitendo namna Serikali inavyotekeleza majukumu yake ya usimamizi wa maafa nchini.
Alisema kuwa mifumo iliyowekwa na Serikali katika ufuatiliaji wa vihatarishi, utoaji wa tahadhari za mapema na uratibu wa operesheni za dharura ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao dhidi ya madhara yatokanayo na maafa mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Bi. Jane Alfred Kikunya, ambaye aliongoza mafunzo hayo, alisema ameridhishwa na hamasa na ari kubwa iliyooneshwa na wanafunzi katika kujifunza masuala ya usimamizi wa maafa na tahadhari ya mapema.
Bi. Jane alieleza kuwa ujio wa wanafunzi hao unaonesha namna sekta ya usimamizi wa maafa inavyoendelea kupata umuhimu katika jamii na taasisi za elimu ya juu. Aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kufungua milango kwa wanafunzi, watafiti na wadau mbalimbali wanaotaka kujifunza kuhusu mifumo ya ufuatiliaji wa majanga, uchambuzi wa vihatarishi, tahadhari za mapema na uratibu wa operesheni za dharura kutembelea ofisi hiyo.
Kwa upande wake, Dkt. Japhet Ringo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma ambaye aliambatana na wanafunzi hao, aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo kuhusu mifumo ya usimamizi wa maafa nchini.
Dkt. Ringo alisema kuwa ziara hiyo imekuwa darasa muhimu lililowawezesha wanafunzi kuunganisha maarifa ya kinadharia wanayojifunza darasani na utekelezaji halisi wa shughuli za usimamizi wa maafa katika ngazi ya Taifa.
Aliongeza kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kitaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza tafiti, ubunifu na maendeleo ya taaluma ya usimamizi wa hatari za maafa ili kusaidia juhudi za Taifa za kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga mbalimbali.


No comments
Post a Comment