WASIRRA AIONYA SERIKALI YA RAIS MAGUFULI,NI KUHUSU OPARESHENI UKUTA,ASEMA NCHI ITAELEKEA KUBAYA,SOMA HAPO KUJUA
Aliyekuwa Waziri wa Kilimo na Chakula na Kada
mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira ameomba wasaidizi wa Rais
John Magufuli kumshauri kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ili kuepusha
madhara yanayoweza kutokea kutokana na maandamano yanayopangwa kufanyika
Septemba 1.
Wassira ameeleza kuwa washauri hao wanapaswa kufanya
hivyo kwani bado nafasi hiyo ipo kuliko kuacha Rais aingie vitani na wananchi
wake kwani madhara yatawapata Watanzania wote.
“Wazungumze ili wasimuingize Rais
kupigana na watu wake kwa maana wote tutapoteza. Kwa nini uweke askari polisi
wote hao, msimweke Rais kwenye vita na watu wake,” Wassira
anakaririwa na Jambo Leo.
“Kinachohitajika ni wasaidizi wa Rais
kumshauri ili kuhakikisha kuwa tofuati zilizopo baina yake na vyama vya
upinzani haziendelei ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika, itafutwe
suluhu,” aliongeza.
Akizungumzia uamuzi wa Serikali kupiga marufuku kufanyika
kwa mikutano na maandamano, alisema kuwa tatizo linaweza kuwa ni aliyekuwa
Mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Alisema kuwa hii inatokana na joto la uchaguzi
lililokuwepo pamoja na nia ya Lowassa kuzunguka nchi nzima kuwashukuru wapiga
kura, kungeweza kuzua tafrani kubwa kwani alipata kura nyingi na alikuwa akidai
ameshinda kwa asilimia 62.
“Ukiwaruhusu kufanya mikutano na
ukwaambia kuwa atakayekuja kutoa shukurani ni Lowassa, ambaye amekuwa akipinga
kushindwa ni sawa na kurejesha hali ya uchaguzi kipindi hiki,” alisema.
Alitaka Serikali kutoa elimu ya wazi kwa umma kuhusu
sababu zinazopelekea kukataza kufanyika kwa mikutano ili kuweka mambo sawa.
“Kama mimi hapa nimetaja sababu kwamba
inawezakana kuwa ni Lowassa. Sasa na wao Serikali waseme tu tunapiga marufuku
mikutano na maandamano… wataje [sababu]na kuzifafanua,” alieleza.
Hata hivyo, Wassira aliwataka Chadema kusitisha
adhma yao na kuhakikisha wanafuata utaratibu ili kupata haki ya kufanya
maandamano na mikutano ambayo alieleza kuwa kila Katiba ya nchi duniani
imeiweka, lakini bila kufuata utaratibu haiwezi kuruhusiwa.