WAGANGA WA TIBA ASILIA WAIBURUZA SERIKALI MAHAKAMANI,NI KWA HATUA YA KUFUTIWA LESENI ZAO,SOMA HAPO KUJUA
MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na Mbadala akiwemo
mmiliki wa Kliniki ya Sure Herbal, Simon Rusigwa wamewasilisha maombi ya kuomba
ruhusa ya kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa leseni za kutoa huduma za
kitabibu.
Wamewasilisha maombi hayo katika Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali na Rusigwa, matabibu wengine waliowasilisha
maombi hayo kupitia kwa Wakili Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah Mandai wa kliniki
ya Mandai Herbalist, Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium na John Lupimo wa
Lupimo Sanitarium.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa jana mbele ya
Jaji Ama–Isario Munisi wa mahakama hiyo, hata hivyo kabla ya kuanza
kusikilizwa, Serikali iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa maombi hayo
hayakufuata misingi ya kisheria.
Katika pingamizi hilo serikali inadai kuwa maombi
hayo yana kasoro kwa kuwa waombaji hawajapita njia zote zinazotakiwa wazifuate
ndipo waende mahakamani pia wanadai maombi hayana miguu ya kusimamia kwa kuwa
hati ya viapo vya walalamikaji vina upungufu ya kisheria.
Baada ya kuwasilishwa kwa pingamizi, Jaji Munisi
aliahirisha shauri hilo hadi kesho saa 8 mchana, ambapo alizitaka pande zote
zinazohusika ziwepo ili kusikiliza pingamizi hilo.
Katika maombi yao, matatibu hao wanadai, wameamua
kupeleka maombi hayo mahakamani, kwa kuwa wanaamini walifutiwa leseni bila
kufuata taratibu za kisheria.
Wamedai wanaamini uamuzi uliochukuliwa umetolewa
bila kupitia Kamati ya Maadili ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, huku
wakidai kuwa huo si uamuzi bali zilikuwa tuhuma mpya, lakini hawakupewa nafasi
ya kusikilizwa.