HESLB YAFUNGUA RASMI DIRISHA LA MAOMBI YA MIKOPO

Na Mussa Augustine, Dar es Salaam
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua rasmi dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 19, 2026, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dkt. Bill Kiwia, amesema dirisha la maombi ya mikopo limeanza rasmi leo na litafungwa Agosti 31 mwaka huu.
Aidha, Dkt. Kiwia amezindua miongozo minne muhimu itakayoongoza utoaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka mpya wa masomo 2026/2027, huku akiwataka waombaji wote kuwasilisha nyaraka sahihi.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu bila vikwazo vya kifedha, huku ikiimarisha usawa katika upatikanaji wa elimu nchini.
“Dirisha la maombi limefunguliwa rasmi kuanzia leo Juni 19,2026 na litabaki wazi kwa siku 73 hadi Agosti 31,2026. Kwa hiyo, waombaji wote watumie muda huu vyema kukamilisha maombi yao kwa usahihi,” amesema Dkt. Kiwia.
Sambamba na kufunguliwa kwa dirisha hilo, HESLB imezindua miongozo minne ya utoaji wa mikopo na ruzuku ambayo imeandaliwa mahsusi kuwawezesha waombaji kuelewa kwa kina masharti, vigezo na taratibu zote zinazohusika katika mchakato wa maombi.
“Miongozo hii imeandaliwa ili kuwasaidia waombaji kuelewa sifa, vigezo na taratibu za kupata mikopo na ruzuku. Tunasisitiza wanafunzi wasome na kuzingatia maelekezo yote yaliyomo kabla ya kuanza kujaza fomu za maombi kupitia mfumo wa OLAMS,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa HESLB, miongozo iliyozinduliwa inahusisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa shahada za awali, stashahada, Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice), pamoja na Mwongozo wa Ruzuku za Samia Scholarship.
Dkt. Kiwia amefafanua kuwa matumizi sahihi ya taarifa binafsi ni moja ya mambo muhimu yatakayochangia maombi kufanikiwa, akisisitiza waombaji kutumia namba sahihi ya mtihani wa Kidato cha Nne waliyoitumia kufanya mitihani yao.
“Namba ya mtihani wa Kidato cha Nne ndiyo itakayotumika katika hatua mbalimbali za uthibitishaji wa taarifa, ikiwemo wakati wa kuomba udahili katika taasisi za elimu ya juu. Hivyo, makosa katika hatua hiyo yanaweza kuathiri mchakato mzima wa maombi,” amesema.
Vilevile, Dkt. Kiwia amewataka waombaji wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea kuhakikisha wanaingiza Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) wakati wa kujaza maombi yao ili kurahisisha uhakiki wa taarifa zao.
Aidha, amewahakikishia waombaji ambao bado hawajafikisha umri huo kuwa hawatanyimwa haki ya kuomba mkopo kutokana na kutokuwa na NIN, kwani mfumo utaendelea kupokea maombi yao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Katika hatua nyingine, amesema kuwa kupitia mpango wa Samia Scholarship, Serikali itaendelea kuwekeza katika kukuza taaluma za sayansi kwa kuwapatia ufadhili wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi kitaaluma.
Amebainisha kuwa wanafunzi 1,000 watakaofanya vizuri zaidi katika tahasusi za sayansi kwenye mtihani wa Kidato cha Sita wa mwaka 2026 watanufaika na ruzuku hiyo maalumu, ambayo imekuwa chachu ya kuongeza ushindani na ubora wa matokeo katika masomo ya sayansi nchini.
“Mpango huu ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta mbalimbali muhimu za maendeleo, ikiwemo afya, teknolojia, uhandisi, kilimo na viwanda,” amesema Dkt. Kiwia.
Ameongeza kuwa HESLB imeweka mikakati ya kuhakikisha waombaji wanapata msaada wa haraka wanapokutana na changamoto katika kipindi chote cha maombi ya mikopo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, Kituo cha Huduma kwa Wateja cha HESLB kitakuwa kinapatikana kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni kwa ajili ya kutoa mwongozo, ushauri na ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati wa maombi.
Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027 linatarajiwa kuwa miongoni mwa hatua muhimu zitakazowezesha vijana wengi zaidi kupata elimu ya juu, huku HESLB ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha hakuna mwanafunzi mwenye sifa anayeshindwa kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha.
No comments
Post a Comment