TWANGE AIPONGEZA WIZARA YA NISHATI KWA KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za nishati unakuwa wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.
Bw. Twange ametoa pongezi hizo Juni 19, 2026 katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma wakati alipotembelea banda la Wizara ya Nishati ambapo ameeleza kuwa mamafanikio yanayopatikana katika sekta ya nishati yanatokana na ushirikiano madhubuti kati ya Wizara ya Nishati na taasisi zake, jambo ambalo limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma na fursa zinazopatikana katika sekta ya nishati ili kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya taifa na kuhakikisha manufaa ya uwekezaji unaofanywa yanafika kwa wananchi wote.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na sekta ya nishati.
Kupitia maonesho hayo, Wizara ya Nishati na taasisi zake zimeendelea kutoa elimu kuhusu miradi ya umeme, gesi asilia na nishati safi ya kupikia, sambamba na kupokea maoni ya wananchi ili kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha sekta ya nishati inaendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa.
No comments
Post a Comment