NI BIFU TU ZANZIBAR,MAALIM SEIF AKIANZISHA NA DK SHEIN,SOMA HAPO KUJUA

MAMBO yanazidi kuharibika. Ndivyo unavyoweza kusema
baada ya Maalim Seif Sharif Hamad kugoma kupokea mkono wa Dk. Ali Mohamed Shein
kwenye msiba wa Alhaj Aboud Jumbe, anaandika Mwandishi Wetu.
Hali hiyo imedhihirisha namna
chuki za kisiasa visiwani humo zilivyotamalaki ambapo Maalim Seif na Dk. Shein
ndio mara ya kwanza kukutana uso kwa uso baada ya Uchaguzi Mkuu wa marudio
uliofanyika tarehe 20 Machi mwaka huu visiwani Zanzibar.
Dk. Shein ndiye aliyekuwa akiongoza mazishi ya Alhaj
Jumbe ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) aliyefariki Jumapili wiki iliyopita.
Kwenye msiba huo, baada ya Dk. Shein kusalimiana na
wageni wengine kwa kuwapa mkono, alipofika kwa Maalim Seif, Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), aligoma kupokea mkono wake.
Baada ya Maalim Seif kutopokea mkono wake, Dk. Shein
aliunyoosha tena kwa matumaini kwamba kiongozi huyo wa CUF angeupokea, hata
hivyo Maalim Seif aligoma.
Kutokana na mgomo huo, Dk. Shein alilazimika kumruka
na kuendelea kusalimiana kwa kupeana mikono na viongozi wengine waliohudhuria
maziko hayo.
Hatua hiyo imepokewa kwa hofu na baadhi ya
waombolezaji waliokuwepo kwenye eneo hilo na walioshuhudia tukio hilo.
Hali hiyo inatafsirika kuwa ni kilele cha chuki za
kisiasa zilizochochewa na Tume ya Uchaguzi visiwani Zanzibar (ZEC) chini ya
mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu kinyume na
Katiba ya visiwa hivyo.
Kabla ya tukio hilo, visiwani Zanzibar kumeripotiwa
kuwepo kwa ubaguzi wa kisiasa katika mambo mbalimbali ikiwemo huduma za kijamii
ambapo wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanalalamika kutengwa na wale wa
CUF.
Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa kuwepo kwa
ubaguzi huo ni katika uuzaji wa bidhaa dukani, usafiri wa daladala pamoja na
vikao vya pamoja vya kijamii.
Mara kadhaa Jeshi la Polisi limekuwa likimwita
Maalim Seif kwa mahojiano kutokana na matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani
humo.
Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani humo wamekuwa
waoga kueleza kiini cha mahojiano hayo ambapo viongozi wa CUF wamekuwa
wakieleza kuwa ni kutokana na tuhuma za uchochezi.
Serikali ya Dk. Shein inayumba kutokana na baadhi ya
Wazanzibari kuipa mgongo kwa tuhuma kwamba, urais aliotunukiwa na NEC hauna
ridhaa ya wananchi wa visiwa hivyo.
Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu
yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia
(bonyeza)> Simgazeti kwa
wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel.