Zinazobamba

ZIMWI LA UBINAFSISHAJI LAMTESA RAIS MKAPA,DHARAU ZAKE KWA NYERERE ZAPELEKEA NBC KUWA HOI ZAIDI NI HAPA

        
UAMUZI tata wa Serikali ya Awamu ya Tatu kubinafsisha Benki ya Taifa ya Biashara (NBC)  kwa kuuza sehemu kubwa ya hisa zake kwa wawekezaji binafsi, umeendelea kuligharimu Taifa, safari hii sababu kubwa ikiwa ni serikali kushindwa kuongeza thamani ya hisa ilizokuwa ikizishikilia takriban asilimia 30 na sasa, kumeibuka shinikizo ili hisa hizo ziuzwe.
           Ubinafsishaji huo kwa njia ya kuuza sehemu kubwa ya hisa za NBC ulipata kupingwa na watu mbalimbali nchini, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere, aliyeamini kwamba ubinafsishaji wa mashirika au taasisi za umma ufanyike kwa taasisi zilizokuwa zikiendeshwa kwa hasara tu na si vinginevyo.

           Habari zinasema thamani ya hisa hizo za Serikali imeporomoka kutokana na Serikali yenyewe kukopa mno ndani ya NBC na kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
         “Hisa za Serikali ndani ya NBC hazina thamani tena kwa sababu serikali imekopa sana kutoka benki hiyo badala ya kuwekeza ili kulinda thamani ya hisa hizo. Imekuwa ikikopa bila kurejesha mikopo yake. Hali ni mbaya na tayari kuna maelekezo yametolewa kwa Benki ya Barclays (mwanahisa mkuu) wasifungue matawi mapya (baada ya kuitwaa NBC) hadi pale serikali itakapouza hisa zake,” kilieleza chanzo chetu cha habari kutoka ofisi ya Msajili wa Hazina kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
           Hali hiyo inajitokeza katika wakati ambao tayari aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, akiwa amekwishapata kuionya serikali mara kadhaa kuhusu matumizi yanayozidi uwezo wa kukusanya kodi, matumizi ambayo fedha zake kwa kiasi kikubwa zinatokana na kukopa katika benki za kibiashara.
         “Mbia mkuu katika hisa za NBC anaishinikiza serikali kuuza hisa zake kwa sababu hazina thamani. Yaani hata zile hela tulizozibana katika NBC nazo zinapotea,” kilieleza chanzo chetu kingine cha habari serikalini kuhusu suala hilo.
         Wakati hali ikiwa hivyo, uongozi wa NBC nchini umekwepa kuzungumzia moja kwa moja suala hilo. Kaimu Meneja Masoko na Masuala ya Biashara wa NBC, Rukia Mtingwa alipoulizwa alijibu; “Hatuwezi kujibu suala la kukisia hasa kama suala hilo linahusu wanahisa wetu.”
         Uongozi wa Wizara ya Fedha nao haukupatikana hadi tunakwenda mitamboni ili kuelezea suala hilo na hata walipotafutwa kwa simu, manaibu mawaziri, Adam Malima na Mwigulu Nchemba, hawakuweza kupatikana, simu zao zikiita bila majibu.
         Kwa sasa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inaitwa National Bank of Commerce (Tanzania) Limited au kwa kifupi NBC (Tanzania) Limited. Ni miongoni mwa benki za biashara nchini zinazoendeshwa chini ya kibali cha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambacho ndicho chombo cha udhibiti wa benki kitaifa.
            Mwanahisa mkuu wa NBC Tanzania Limited, Barclays Africa Group Limited imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa Johannesburg na hivi sasa nchini wanamiliki NBC Tanzania Limited na Benki ya Barclays Tanzania.
          Wataalamu wa masuala ya kibenki wanadhani shinikizo hilo la kutaka hisa za serikali ziuzwe ni katika mchakato wa kuziunganisha benki hizo mbili za biashara baada ya kuona shughuli za benki mojawapo kati ya hizo inakabiliwa na changamoto kadhaa. 
         Taarifa kadhaa zinabainisha kwamba hadi kufikia Desemba mwaka 2013, NBC (Tanzania) ilikuwa kati ya taasisi kubwa ya utoaji huduma za fedha nchini, ikikadiriwa kuwa na mali ya thamani (asset valuation) ya takriban Dola za Marekani milioni 994 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.587 na hisa zisizo na riba ya kudumu kwa wanahisa wake zinazokadiriwa kuwa dola za Marekani milioni 120.4 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 195.
         Kwa kuzingatia takwimu hizo za mwaka jana, ilikuwa ni benki ya nne kimtaji katika biashara, nyuma ya Benki ya National Microfinance (NMB), Benki ya CRDB na Benki ya FBME.
          Historia ya kuanzishwa kwa benki hiyo inaanzia mwaka 1967 pale Serikali ya Tanzania ilipofanya uamuzi wa kutaifisha taasisi za fedha, kuwa mali ya umma, zikiwamo benki.
        Mwaka 1997, benki hiyo iligawanywa katika taasisi tatu: Mosi, NBC Holding Corporation; pili; National Microfinance Bank (NMB) na tatu; NBC (1997) Limited.
Mwaka 2000, Kundi la Kibenki la Afrika Kusini, Barclays Africa Group, kwa wakati huo likijulikana kama Absa Group Limited, lilinunua sehemu kubwa ya hisa za NBC (1997) Limited na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilibakiwa na asilimia 30 ya hisa wakati mwanahisa mwngine, International Finance Corporation (IFC) kutoka World Bank Group likiwa na hisa asilimia 15. Kutokana na mauzo hayo ya hisa, benki hiyo ikaitwa National Bank of Commerce (Tanzania) Limited.
Jedwali la Umiliki wa hisa NBC kwa sasa
National Bank of Commerce (Tanzania) Stock Ownership
Rank
Name of Owner
Percentage Ownership
1
External Links icon
55.0
2
External Links icon
30.0
3
External Links icon
15.0
4
TOTAL
100.0
 Misuli ya Barclays Africa Group
The Barclays Africa Group, ambayo awali iliitwa Absa Group Limited, ni kati ya taasisi ya kibenki yenye nguvu Afrika Kusini, ikiwa na mali zinazozidi dola za Marekani bilioni 77 kwa mujibu wa taarifa za Juni, mwaka 2013.
Katika uendeshaji wa shughuli zake za kibenki, taasisi hiyo imekuwa ikiendesha shughuli zake katika nchi kadhaa kwa njia ya ubia, zikiwamo Angola, Msumbiji, Tanzania, Namibia na Zimbabwe.
Ukubwa wa NBC Tanzania
Kwa kuzingatia takwimu za hadi kufikia Oktoba mwaka 2013, NBC Bank Tanzania ilikuwa na matawi yaliyosambaa maeneo mbalimbali nchini, katika miji mikubwa na midogo, matawi hayo yakitajwa kuwa ni zaidi ya 90.

Kwa sasa, Mwenyekiti wa Bodi ya NBC ni Dk. Mussa Assad wakati Mkurugenzi Mtendaji wake akiwa, Mizinga Melu, mwanamama aliyeteuliwa katika wadhifa huo Mei 20, mwaka 2013, akitokea katika wadhifa wa ofisa kutoka Benki ya Standard Chartered nchini Zambia.

Hakuna maoni