JAJI WARIOBA AUNGANA NA UKAWA KUTUMIA NGUVU YA UMMA KUIPINGA KATIBA YA SAMWEL SITTA,SOMA HAPA
Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametangaza rasmi kuungana na umma
mpana, kupinga rasimu ya Katiba Mpya inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba
(BMK).
Hatua hiyo
isiyotarajiwa, inafuatia Bunge Maalum la Katiba kukamilisha rasimu hiyo
Jumatano iliyopita, ikitarajiwa kupigiwa kura mapema wiki ijayo.
Akizungumza
kwenye adhimisho la miaka 19 tangu kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Aidha, Jaji Warioba, alisema Bunge hilo limeondoa mambo ya
msingi yaliyopendekezwa na wananchi yakiwa ni kiini cha kupatikana kwa
Katiba Mpya.
Adhimisho hilo
lilitumika pia kumkumbuka muasisi wa LHRC, marehemu Dk. Sengondo Mvungi, ambapo
kitabu kinachoelezea maisha yake, kinachoitwa ‘Sengondo Mvungi, breathing the
Constitution’ ikimaanisha, ‘Sengondo Mvungi, pumzi ya Katiba’,
kilizinduliwa.
Kwa mujibu wa Jaji
Warioba, rasimu ya Katiba inayopendekezwa na BMK ni mfano wa ile iliyopo sasa
ikiwa imewekewa viraka.
“Bunge limeacha
mawazo ya wananchi na kuingia katika mikakati na misimamo yao, walioona rasimu
yetu siyo, watatoka bungeni watakutana nasi mitaani, tutatetea maoni ya
wananchi na wao watoke waje kutetea mawazo yao,” alisema.
Jaji Warioba, alitoa
mfano wa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni ya wananchi, yakaondolewa na BMK
kuwa ni maadili, tunu za taifa, mgawanyiko wa madaraka, miiko ya uongozi
na Muungano.
MAADILI
Jaji Warioba, alisema wananchi waliotoa maoni walisisitiza
masuala yanayohusu maadili kwa taifa yaingizwe kwenye Katiba Mpya, lakini hali
hiyo haikukubalika kwa BMK.
Kadhalika, alisema
tunu za Taifa ambazo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya taifa zilizopendekezwa na wananchi, rasimu hiyo ya bunge
imezipunguza na kubaki nne tu.
Alizitaja
zilizowasilishwa na rasimu ya bunge kuwa ni lugha ya Kiswahili, muungano, utu
na udugu na amani na utulivu.
“Tunu za taifa
zilizopendekezwa na wananchi, na siyo vyama vya siasa wala tume zimeondolewa,
Bunge linasema eti ni hiyo ni misingi ya utawala,” alisema.
Aliongeza, “mimi siwaelewi kabisa kusema hizo siyo tunu za
kitaifa, siwaelewi kabisa,” alisema.
Alisema, sura ya
tatu ya rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume yake, ilihusu miiko ya
uongozi.
Jaji Warioba,
alisema sura hiyo ilieleza kuwa kiongozi wa umma hapaswi kuwa na akaunti ya
benki nje ya nchi na kutangaza mali na madeni yake.
Pia, ilieleza
kiongozi huyo anapaswa kuwasilisha kwenye ofisi za umma zawadi anazopewa,
kutotumia mali za umma kwa mambo binafsi, kukomesha rushwa na ufisadi.
Alisema, miiko ya
uongozi ilifanikisha kukabiliana na kadhia kama Ufilipino, Kenya, Namibia na Afrika
Kusini.
“Tunajua ufisadi na
rushwa ndiyo chanzo cha hayo yote, watu wanapewa zawadi wanasaini mikataba ya
hovyo, lakini tunapokuwa na miiko yeyote atakayebainika amepokea zawadi au ana
akaunti nje ya nchi atawajibishwa… kwenye haya wameniita mimi ni shida,”
alisema.
MADARAKA YA NCHI
Jaji Warioba, alisema wananchi walipendekeza kumuondoa
Mwakilishi asiyewajibika kwao, kuwapo ukomo wa ubunge na muundo wa
serikali tatu, lakini vimeondolewa na BMK.
“Wananchi walisema
baadhi ya wabunge ni watalii kwenye majimbo yao, wakataka wapate mamlaka ya
kuwaondoa, cha ajabu wenyewe wamejipa mamlaka ya kumfukuza mbunge asiyeshiriki
kikao kimoja, na vyama vya siasa vimejipa madaraka ya kuwaondoa wabunge wao,
kwa nini mwananchi anyimwe hili,” alihoji.
MGAWANYO WA MADARAKA
Alisema, Tume ilipendekeza kuwa kutokana na mwingiliano uliopo
kati ya Bunge na Serikali, ipo haja ya kuwapo mgawanyo wa madaraka kwenye
Katiba Mpya.
Alitoa mfano namna ushawishi wa Rais ulivyofanikishwa kurejeshwa
bungeni kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kukutana na viongozi wa
upinzani.
Aliongeza, “hata sasa, wakati rasimu yao inasema Katiba itaitwa
ya mwaka 2014, Rais anasema haiwezi kupatikana mwaka huu hadi 2016. Huu ni
muingiliano wa madaraka, ndio maana tume tuliona kila mhimili
ujitegemee.”
MUUNGANO
Jaji Warioba, alisema muundo wa serikali tatu ulipendekezwa na
wananchi na kwamba ndani ya Tume, kila mjumbe alikuwa na maoni yake.
“Mfano Baregu (Profesa Mwesiga Baregu) alitaka serikali mbili,
Joseph Butiku alitaka moja, Awadhi Said alikuwa muumini wa Muungano wa mkataba,
mimi ni serikali mbili kwenda moja,” alisema.
AZIPONDA KURA ZA MTANDAO
Jaji Warioba, alisema pamoja na kasoro iliyopo kupigia kura
ibara badala ya sura za rasimu ya Katiba inayopendekezwa, alipinga pia utaratibu
wa kuruhusu wajumbe wasiokuwapo bungeni kupiga kura.
“Kusaka kura kwa mtandao hakuwezi kutuletea Katiba ya maridhiano
na mimi nimeanza kukata tamaa, ninachoona mchakato huu utarudiwa mara
baada ya kupatikana kwa Rais mpya,” alisema na kuongeza:
LHRC BILA DK. MVUNGI
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema
endapo angekuwapo Dk. Mvungi, angeshangaa kuona maslahi ya taifa yanatupwa na
yale ya itikadi yanapewa kipaumbele.
Pia, alisema
angeshangaa kuondolewa kwa vipengele kama kuwajibishwa wabunge, ukomo wao
na jinsi mchakato ulivyokiuka maoni ya wananchi.
Mjane wa Dk. Mvungi,
Anna Mvungi, alisema baada ya kuteuliwa katika tume, moja ya kauli zake (Dk.
Mvungi) ilikuwa ni ‘nimetimiza nia yangu’.
Mwenyekiti wa ukoo wa
Mvungi, Adrian Mvungi, aliiasa LHRC kuondokana na woga na kuendeleza mapambano
ya kutetea haki za watu.
Mmoja wa wahariri wa
kitabu hicho, Profesa Chris Maina, alisema Dk. Mvungi alikuwa ni Profesa
kutokana na makala 20 alizoziandika kwa wananchi na shauri kuhusu wanyonge na
matatizo wanayoyapata. Kuhusu Tume ya Warioba, alisema pamoja na `madongo’
wanayoyapa wamekuwa imara kutokana na yote waliyosimamia waliyaamini.
“Jinsi tunavyopata
vioja vya Dodoma tunazidi kuvumbua ubora wa tume hii, wananchi wanajua mchele
na pumba historia haifutwi na FFU,” alisema.
Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia, alisema kuna
mazungumzo yanayoendelea yakivihusisha vyama vya siasa hususani vyenye wabunge,
ili kuinusuru Katiba Mpya.
“Yapo mazungumzo yanayoendelea yanahusisha vyama vyote vyenye
wawakilishi bungeni CCM, Chadema na NCCR-Mageuzi, tunataka Tanzania isifike
mahali tukamwaga damu kwa sababu ya ubinafsi wa watu wachache,” alisema.
KITABU CHA DK. MVUNGI
Katika kitabu hicho zipo makala mbalimbali za wanataaluma,
familia na wanafunzi na walimu wake, wananchi na wanahabari ambazo zimemuelezea
jinsi alivyofanya kazi za utetezi wa wanyonge.
Kitabu hicho
ambacho kimepambwa na picha 157 kina sura kumi ambazo waandishi wake wametumia
lugha mbalimbali kufikisha ujumbe ambazo ni Kiswahili, Kingereza, Kijerumani na
Kipare kilichokuwa lugha ya Dk. Mvungi.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni