HILI HAPA TAMKO LA WANAHARAKATI NGAZI YA JAMII KUHUSU RASM YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA NA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Wanaharakati wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa
la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao
tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi wa kina wa Rasimu iliopendekezwa
na kutolewa na Bunge maalum la Katiba tarehe 24/9/2014 mjini Dodoma. Tamko hili
tunalitoa kwa kuhusianisha rasimu ya Katiba iliopendekezwa na madai ya wanaharakati wa Masuala ya Jinsia.
Wanaharakati masuala ya jinsia na haki za binadamu
waliainisha madai 12 ya kikatiba yanayowahusu Wanawake na makundi mengine ya
walio pembezoni. Madai hayo ni pamoja na Haki za wanawake zibainishwe kwenye
Katiba, Sheria Kandamizi zibatilishwe, Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na
kumiliki rasilimali ya nchi, Utu wa mwanamke ulindwe, Utekelezaji wa mikataba
ya kimataifa kuhusu haki za Wanawake, Haki sawa katika nafasi za uongozi, Haki
za wanawake wenye ulemavu, Haki ya uzazi salama, Haki za watoto wa kike, Haki
ya kufikia na kufaidi huduma za Msingi, Wajibu wa wazazi katika matunzo ya
watoto na Katiba iunde chombo maaalum kitakachosimamia haki za wanawake katika
maeneo yote ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi.
Tunapongeza kamati ya uandishi wa katiba na Bunge
maalum la katiba kwa kuzingatia na kutambua umuhimu wa baadhi ya masuala ya
Jinsia na kuyaingiza katika rasimu ya Katiba lakini tumeshangazwa kuona suala
la maji halijatambuliwa kama haki ya msingi ya kikatiba wakati ambapo 65% ya
watu wa mijini ndio wanapata maji safi na salama huku 42% ya wakazi wa vijijini
ndio wanaopata maji safi na salama. Tunadai haki ya kupata maji safi na salama
iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea
umbali mrefu wa kutafuta maji.
Rasimu ya katiba imeipa uwezo bunge la jamhuri ya
muungano kumuwajibisha Rais pindi akishindwa kutekeleza majukumu yake na
akienda kinyume na sheria na taratibu za nchi. Lakini rasimu hii imewanyima wananchi haki yao ya msingi ya kumuwajibisha kiongozi
(Mbunge/diwani) waliemchagua kwa kura zao halali pindi anaposhindwa kutekeleza
majukumu na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni kwa wananchi. Tunadai rasimu hii
ya katiba iweke ukomo wa vipindi kwa wabunge kukaa madarakani na iweke mfumo
mzuri wa wananchi kuwawajibisha viongozi
wasiotimiza majukumu yao kama ilivyo kwa bunge ilivyopewa dhamana na haki ya
kumuwajibisha Rais anaposhindwa kutimiza wajibu wake.
Tunapongeza bunge maalum la katiba kwa kupunguza umri
wa kugombea Urais kutoka miaka 45 ya zamani hadi miaka 40 kwa sasa (Ibara 85)
na kuweka utaratibu wa kuhoji matokeo ya urais katika mahakama kuu. Hali hii
itasaidia kutoa haki kwa vijana na
wanawake kushiriki katika kuwania nafasi za uongozi na pia itawezesha wananchi wenye
malalamiko dhidi ya matokeo ya Urais
kupata haki ya kukata rufaa na kupinga matokeo.
Rasimu hii ibara ya 79 na 80 imeendeleza kumlimbikizia Rais madaraka ya
kuteua viongozi na watendaji mbalimbali
wa serikali bila ya kufuata na kuzingatia ushauri atakaopewa na mtu au mamlaka yoyote. Hali hii bado inaendeleza mfumo mbaya wa
mgawanyo wa madaraka kikatiba na inaendeleza mfumo kandamizi katika utoaji wa
fursa za kiuongozi. Tunashauri rasimu hii ya Katiba iweke ukomo wa uteuzi kwa
rais ili kutoa fursa kwa mamlaka nyingine kufanya uteuzi wenye tija. Mfano
katiba ya Kenya imetoa fursa ya wananchi kuhoji uteuzi unaofanywa katika ngazi
mbali mbali.
Ibara ya 135 (b) imeeleza sifa ya mbunge awe anajua
kusoma na kuandika Kiswahili au kingereza. Sifa hii ya kuchaguliwa kuwa mbunge
inadidimiza maendeleo ya taifa kwani bunge linatakiwa kupitia mikataba mbali
mbali ambayo kwa sehemu kubwa ipo kwenye lugha ya kingereza. Je kigezo hiki cha kujua kusoma na kuandika
kwa mbunge kutaweza kumfanya aweze kuisimamia na kuiwajibisha serikali
kikamilifu? Na je kwa kigezo na sifa hizi za mbunge je itaondoa tatizo la nchi
kuingia mikataba mibovu? Tunadai rasimu hii ya katiba ibadilishe sifa ya
kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne.
Tunapongeza bunge maalumu la Katiba kwa kutambua haki
ya upatikanaji wa huduma bora ya afya
kwa watu wote ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi salama (Ibara ya 14 (2) (f) ),
lakini rasimu hii bado haijaonesha ni namna gani makundi ya walio pembezoni
kama wanawake, wazee na walemavu wataweza kufikia huduma bora za afya bila
vikwazo kutoka kwa watoa huduma hizo. Kwa mfano rasimu hii haijaonesha namna
gani wanawake wajawazito, walemavu na wazee wataweza kupata misamaha ya
kuchangia gharama za upatikanaji wa
huduma za afya. Tunadai rasimu iweke mfumo mzuri wa kuwasaidia makundi ya walio
pembezoni kuweza kupata huduma bora za afya bila ya kikwazo.
Ibara ya 111 (1) (d) imetaja sifa ya kuwa waziri au
naibu waziri kuwa ni lazima awe ni mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu hiki kinaendeleza mgongano wa madaraka kati mihili mikuu miwili ya dola
(Bunge na Serikali) kwa kumpa madaraka mbunge kuwa waziri au naibu waziri.
Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge ili kuimarisha utendaji na
uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili kujitegemea
Katika ibara 22 (2) (d) imeanisha haki ya wanawake
kupata, kumiliki, kutumia, kuendeleza na kusimamia ardhi kama ilivyo kwa
mwanaume lakini tumeshangaa kuona katika ibara ya 22(2) (b) rasimu hii ikitoa
fursa ya bila ya ukomo kwa wawekezaji kuweza kutumia ardhi kwa ajili ya
maendeleo ya kiuchumi na makaazi. Tunashauri kipengele hiki kiweke ukomo kwa
wawekezaji kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya kimaslahi
na ya kikatiba kati ya wananchi na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa
ardhi.
Tunapongeza bunge maalum la katiba kwa kutambua haki
za wanawake na usawa wa kijinsia katika ushiriki na upatikanaji wa fursa sawa
za ajira, ushiriki katika ngazi za
maamuzi, kumiliki mali na kupata ujira sawa na mwanaume katika kazi zenye sifa
zinazofanana (Ibara ya 54 kifungu A hadi G). Lakini rasimu hii bado haijatamka
wazi uwiano wa asilimia 50 kwa 50 katika ngazi na nafasi mbali mbali za maamuzi.
Tunadai katiba itamke uwiano wa 50/50 katika nafasi na ngazi zote za maamuzi.
Ibara ya 14 (2)(e) imeeleza katiba itaweka
utaratibu unaofaa kwa ajili ya kila mtu
kupata elimu, lakini ibara 49(1)
imeeleza haki ya kupata elimu ya msingi inayomtayarisha kikamilifu kuendelea na
elimu ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanza kujitegemea. Tunadai
rasimu ya katiba itambue haki ya kupata elimu kutoka elimu ya awali hadi elimu
ya juu ili kuweza kuondoa matabaka katika jamii na sio kuweka utaratibu tu wa
upatikanaji wa elimu.
Ibara ya 257 (3) kimetoa uhuru kwa Benki kuu ya
Tanzania (BOT) kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa, kudhibitiwa au
kupewa maelekezo na mtu au mamlaka yoyote. Kifungu hiki kinakinzana na dhana
bora ya uwajibikaji na utawala bora na kinatoa mwanya wa ubadhirifu na matumizi
ya mabaya ya fedha za umma kwa kigezo cha watendaji wa benki kuu kutowajibishwa
kutokana na makosa yao kiutendaji pindi wanapokua madarakani. Kifungu hiki
kinachochea na kutoa fursa ya ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali na fedha za
umma. Tunadai ibara hii irekebishwe.
Kutokana na hayo tulio yaeleza hapo juu tunadai
yafuatayo;
i.
Tunadai katiba itamke uwiano wa 50/50 katika
nafasi na ngazi zote za maamuzi kati ya wanawake na wanaume kuanzia ngazi za
chini kabisa hadi taifa.
ii.
Tunadai
haki ya kupata maji safi na salama iwe ni haki ya kikatiba ili kuweza
kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutembea umbali mrefu wa kutafuta maji.
iii.
Tunadai rasimu hii ya katiba ibadilishe
sifa ya kiwango cha elimu ya mbunge kuwa kidato cha nne.
iv.
Tunadai mawaziri wasiwe miongoni mwa wabunge
ili kuimarisha utendaji na uwajibikaji wa mihimili yote mitatu kwa kila mhimili
kujitegemea.
v.
Tunadai katiba iweke ukomo wa vipindi kwa
wabunge kukaa madakani na iweke mfumo mzuri wa kuwawajibisha viongozi
wasiotimiza majukumu yao kwa wananchi.
vi.
Tunadai rasimu iweke mfumo mzuri wa
kuwasaidia makundi ya walio pembezoni kuweza kupata huduma bora za afya bila ya
kikwazo.
vii.
Tunadai kipengele cha ukomo kwa wawekezaji
kutumia ardhi ili kuweza kuepusha migongano na migogoro ya ardhi kati ya wananchi
na wawekezaji katika suala zima la umiliki wa ardhi.
viii.
Tunadai katiba iunde chombo maaalum
kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa, na
kiuchumi
ix.
Tunadai rasimu ya katiba itambue haki ya
kupata elimu kutoka elimu ya awali hadi elimu ya juu ili kuweza kuondoa
matabaka katika jamii na sio kuweka utaratibu tu wa upatikanaji wa elimu.
x.
Tunadai rasimu hii ya katiba ifute
kipengele cha Benki kuu ya Tanzania (BOT) kutowajibishwa na kudhibitiwa na mtu au mamlaka yoyote ya kiutendaji ili
kuimarisha mfumo wa uwajibikaji.
Tamko hili limesainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TGNP Mtandao kwa niaba ya washiriki wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) na
wanaharakati wa ngazi ya jamii leo
tarehe 27/9/2014.
Lilian Liundi
TGNP Mtandao
.................................
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Kamati ya uchambuzi wa rasimu inayopendekezwa ni hawa
wafuatao;
i.
Badi
Darusi Mwenyekiti
ii.
Esther
William Katibu
iii.
Hamadi
Masudi Mjumbe
iv.
Rehema
Mayuya Mjumbe
v.
Heriet
Kabende Mjumbe
vi.
Lena
Jackson Mjumbe
vii.
Selemani
Bishagazi Mjumbe
Hakuna maoni
Chapisha Maoni