RC CHALAMILA AZINDUA OFISI YA WAMACHINGA NA BODABODA MKOA WA DAR
RC Chalamila(mwenye kibaragashia) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Ofisi ya Wamachinga na Boodaboda Mkoa wa Dar es salaam.
*Amshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha ujenzi wa ofisi hiyo.
*Awataka Wamachinga na Bodaboda kuitumia ofisi hiyo kwa tija ili kufanikisha malengo yao.
Na Mwandishi Wetu,
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mh. Albert Chalamila, leo Machi 13, 2025, amezindua ofisi itakayotumiwa na Wamachinga pamoja na maafiaa usafirishaji (Bodaboda) Mkoa wa Dar es salaam,iliyojengwa katika eneo la Wakala wa Majengo (TBA) Magomeni Kota, Wilayani Kinondoni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Chalamila amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo pamoja na miradi mingine inayotekelezwa ndani ya mkoa huo.
Aidha amesema kuwa furaha ya Rais Samia ni kuona Watanzania wananufaika moja kwa moja na miradi hiyo ili kujenga jamii yenye ustawi.
RC Chalamila amesema kuwa ofisi hiyo itatumika kuwahudumia machinga pamoja na bodaboda wa mkoa huo, huku akiyataka makundi hayo kuitumia kwa tija ili kufanikisha maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.
Naye Bi Zubeda Masoud, akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. Toba Nguvila, amesema kuwa ujenzi wa ofisi hiyo umetokana na maagizo ya Rais Samia kwamba kila mkoa uwe na ofisi ya machinga. Kwa msingi huo, serikali kupitia OR-TAMISEMI ilitoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo, ambayo sasa imekamilika na kuzinduliwa rasmi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufanikisha ujenzi wa ofisi hiyo na kuahidi kuwa kama wilaya, watahakikisha wanakamilisha mahitaji mengine muhimu, ikiwemo samani na kompyuta, ili kuwezesha utendaji kazi wa kisasa.

Post Comment
Hakuna maoni
Chapisha Maoni