Zinazobamba

TAMISEMI YATOA TAARIFA NZITO KUHUSU WANAFUNZI WALIOFAHURU MASOMO YA SAYANSI,



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI JUU YA WANAFUNZI WALIOFAULU MASOMO YA SAYANSI
                         
1.0.         UTANGULIZI                 

Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu katika fani za sayansi kwa kujiwekea  mkakati wa kuhakikisha kuwa kila Mwanafunzi aliyefaulu masomo ya sayansi anapangiwa tahasusi (Combination) ya masomo ya sayansi.

Katika matokeo ya mtihani kwa mwaka 2014,  inaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 22,685  kati yao  Wasichana 7,859 na Wavulana 14,826 wamechaguliwa kusoma tahasusi za sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746  kati yao Wasichana 5,038 na Wavulana 13,708 kwa mwaka 2013.

Uchaguzi wa wanafunzi kidato cha tano kwa mwaka 2014 ulifanyika mwezi mei, 2014 na matokeo yake kutangazwa kupitia tovuti ya OWM- TAMISEMI mwezi Juni 2014.

Tofauti na miaka mingine iliyopita, Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I -III umeongezeka kutoka watahiniwa 35,357 mwaka 2012 hadi 71,527  mwaka huu. Ufaulu huu ni zaidi ya asilimia mia moja ya watahiniwa waliokuwa na sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka 2013.

Natoa pongezi nyingi kwa walimu, wanafunzi,wazazi/walezi na wadau wote wa elimu kwa juhudi walizozifanya kuwezesha ufaulu katika masomo ya sayansi kuongezeka kwa kiasi cha kuridhisha.

Matokeo haya yanakaribia sana malengo ambayo Serikali imejiwekea  kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (yaani Big Results Now-BRN) ambapo serikali ilijiwekea  lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa asilimia 60 mwaka 2013. Matokeo halisi yanaonyesha kuwa ufaulu umepanda kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.


Yapo manufaa mbalimbali ambayo yatapatikana kutokana na ufaulu huu wa wanafunzi kwa taifa na kwa wanafunzi husika. Kwa taifa ufaulu katika masomo ya sayansi utasaidia kupunguza uhaba wa wataalamu katika fani mbalimbali za sayansi na pia unarahisisha kazi ya kuwapatia wanafunzi nafasi mbalimbali za kujiendeleza katika masomo ya ngazi ya juu.

Kwa upande wa wanafunzi, kufaulu vizuri kunawawezesha kuendelea na masomo ya juu, inasaidia kuwapatia nafasi ya uchaguzi wa fani ambazo wangependa kusomea na pia inawajengea kujiamini kuwa wanaweza kufanya vizuri.


2.0.          UCHAGUZI WA WANAFUNZI  WA KIDATO CHA TANO
           MWAKA  2014.

Wanafunzi 54,058 sawa na asilimia 75.61 ya wanafunzi 71,527 wamechaguliwa awamu ya kwanza kujiunga kidato cha tanoTanzania Bara kwa mwaka 2014. Aidha wanafunzi 472 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi.

Uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha tano katika shule za sekondari za serikali na vyuo vya ufundi kwa mwaka 2014 umefanywa kwa kuzingatia taratibu zifuatazo:-
                   i.            Kila mwanafunzi kuwa na fursa ya kuchagua shule na tahasusi tano kwa mtiririko wa vipaumbele vyake;
                 ii.            Mfumo wa kielectroniki umetumika ambao umeoanishwa na matokeo ya mtihani ya watahiniwa wa kuhitimu Elimu ya Sekondari, tahasusi (combination) na shule walizochagua kwa kutumia Selform walizojaza wakiwa shuleni;
              iii.            Mfumo wa kieletroniki umewapangia wanafunzi kwenda kidato cha tano kulingana na sifa, nafasi kwa kila tahasusi na shule, machaguo ya wanafunzi yaliyoko kwenye selform na mahali anapotoka mwanafuzi;
              iv.            Wanafunzi ambao wamefaulu kwa sifa ya kwenda kidato cha tano lakini tahasusi zote tano walizochagua hazikukidhi vigezo (cut-off points) na ambao hawakujaza Selform jambo lililosababisha mfumo  kutotambua machaguo yao (shule  na tahasusi), mfumo umewachagulia tahasusi na shule;
                 v.            Wanafunzi 22,685 (wasichana 7,859 na wavulana 14,826) mwaka 2014 wamechaguliwa kusoma tahasusi za sayansi ikilinganishwa na 18,746 (wasichana 5,038 na wavulana 13,708) mwaka 2013, uchaguzi huu uzingatia ufaulu, machaguo yao na nafasi zilizopo katika shule husika;
              vi.            Hadi 14 Julai 2014, Wanafunzi 1,518 wamebadilishiwa shule na tahasusi kati ya 3,478 walioomba kubadilishiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiafya;

3.0.           CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA 
                   i.   Wanafunzi kuomba kubadilishiwa tahasusi na shule tofauti na zile walizochagua awali;
                 ii.   Ufaulu wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na kidato cha tano kutowiana na nafasi  zilizopo;

4.0.          HITIMISHO

Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi kusoma  masomo hayo,  imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati. Aidha, Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kwa wanafunzi waliobaki  kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za kidato cha tano, baada ya kubaini uwepo wa nafasi hizo; na tunatarajia kwamba baadhi ya wanafunzi wenye sifa watachaguliwa kwenda kusomea ualimu.

Wanafunzi ambao wamefaulu vizuri masomo ya sayansi na wanapenda kusoma masomo hayo wanayofursa ya kubadilisha tahasusi endapo kwenye shule walizopangwa kupitia kwa wakuu wao wa shule.  Endapo tahasusi hawafundishi kene shule hizo wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa Maafisa elimu Mikoa ambayo shule hizo zipo kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa ili waweze kubadilishiwa tahasusi za sayansi kwenye shule zilizopo kwenye Mikoa husika.

Aidha, Jamii inaweza kuwasiliana na watendaji wa Wizara na Mikoa kwa simu ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI .  Hivyo, naendelea kuwasisitiza watendaJi wote wa elimu hususani Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Mikoa kusimamia utekelezaji wa suala hili.  Lengo la Serikali ni kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanao soma masomo ya sayansi ili kuendana na malengo ya Melenia na kutekeleza Mpango wa BRN.

Vilevile, Serikali inaendelea kusisitiza kila mwanafunzi kwenda kuripoti shule aliyopangiwa kuanzia tarehe 10-30 Julai 2014, orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti za www.pmoralg.go.tz na www.moe.go.tz.

IMETOLEWA NA NDG. JUMANNE SAGINI, KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA.




No comments