Zinazobamba

NJAMA ZA CCM,KUIMALIZA KABISA CHADEMA ZAZIDI KUFICHUKA,SOMA HAPA KUJUA NJAMA HIZO

                            

     Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Freeman Mbowe Picha na Maktaba,

 Na Shabani Matutu kutoka Gazeti la Tanzania Daima

HOFU ya kung’oka madarakani iliyojengeka kwa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wasiokuwa waadilifu imeelezwa kuwa sababu ya kudhoofisha vyama vya upinzani nchini.
        Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima Jumapili, viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani nchini wamesema kwamba CCM wanahakikisha wanatumia gharama kubwa kujilinda ili wabaki madarakani.
      Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema kila unapokaribia uchaguzi wa vyama au wa kitaifa, chama tawala hupanga mikakati ya kuvisambaratisha vyama tishio.
     
     “Viongozi wengi walioko madarakani wamekuwa hawataki kuona wanaondolewa katika nafasi wanazoshikilia kutokana na kuhofia kwamba chama kingine kikiingia madarakani, makosa yao yataonekana, hivyo usalama wao wanauona utakuwa shakani kutokana na tuhuma wanazokuwa wanatuhumiwa nazo, wanaweza kupelekwa mahakamani,” alisema.
         Dk. Slaa, aliongeza kuwa hofu hiyo inasababisha viongozi hao kutafuta mbinu mbalimbali za kuvidhoofisha vyama hivyo, ikiwamo kuviwekea kwa makusudi mamluki kwa nia ya kuvivuruga.
          “Mambo hayo ya kuvihujumu vyama vinavyokuwa imara yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika historia ya vyama vya Tanzania. Baadhi ya vyama ambavyo vimewahi kukutana na hujuma hiyo ni pamoja na CUF, NCCR –Mageuzi na sasa CHADEMA ambayo imehusishwa na propaganda zote mpaka ugaidi, kwani hivyo ni vitu vya kawaida kama vikizoeleka, kwani mti wenye matunda ndio hupigwa mawe,” alisema.
       Aliongeza kuwa CHADEMA hivi sasa imekuwa ikishambuliwa kwa madai ya kukiuka katiba yake, lakini kutokana na uongozi imara uliopo fitna hizo hazitofanikiwa.
      Alisema vyama vya upinzani vinapotengeneza viongozi imara hujiwekea hazina ya kukabiliana na mashambulizi ya hovyo kama yafanywayo na CCM.
       “Tofauti na wengi wanavyofikiri kwamba mapito tunayopita yanadhoofisha, si kweli, ila naamini mtadhoofika kama mko dhaifu, mtadhoofika kama yale yanayosemwa yapo, mtadhoofika kama hamna mipango na lengo madhubuti mnalolipigania, na mkiwa wa Mungu hakuna hujuma yoyote itakayoshinda,” alisema Dk. Slaa.
          Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema kuwa hiyo ni mikakati inayopangwa kwa makusudi na CCM, kwa nia ya kudhoofisha demokrasia nchini.
        Alisema kuwa anashangazwa na ambavyo CCM imekuwa ikishughulikia vyama vya siasa kwa nia ya kuua upinzani nchini.
       Sakaya alibainisha kwamba CCM imekuwa ikitumia njia mbalimbali kudhoofisha vyama vya siasa vyenye nguvu kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuingilia mambo ya ndani ya CHADEMA.
          Alisema mara kadhaa msajili wa amekuwa akiingilia chaguzi za ndani za vyama vya siasa hususani vya upinzani, si kwa lengo la kuvirekebisha bali kuvivuruga na kutoa mwanya kwa chama tawala kubakia madarakani.
     “Msajili amesahau kwamba majukumu yake hayakuwa kuangalia nani anayestahili kugombea nafasi fulani katika chama, nimeshangaa sana kuona amefikia hatua kuingilia uchaguzi wa ndani wa vyama na kusema fulani na fulani wasigombee.
           “Hilo linanipatia shaka huko tuendako, itafikia wakati tutachaguliwa mtu wa kugombea katika vyama na msajili, tukiruhusu mambo kama haya yaendelee, tujue kwamba tunakwenda kuua demokrasia nchini, tusingependa vyama viingiliwe ndani na ndiyo maana vina sera, falsafa na taratibu za kuendesha mambo yao, na kama kinafanya makosa zipo sheria za kufuata,” alisema Sakaya.
Alielezea hofu yake kuhusu utendaji wa msajili wa vyama vya siasa kutokana na ukweli kwamba tangu ateuliwe hajamaliza hata mwaka mmoja, anaanza sasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa.
“Amesahau majukumu aliyowekewa hapo kuwa ni kuhakikisha vyama vya siasa vinashamiri na kuota mizizi, sasa inashangaza kuona anafanya mambo ya kuvidumaza,” alisema.
     Aliongeza kuwa kazi ya msajili ni kusimamia katiba ya chama kama inafuatwa na si kuangalia mgombea anayestahili kugombea nafasi yoyote katika chama.
      “Kama tukiruhusu haya tunakwenda kuua vyama vya upinzani, mimi nahisi kuna mbinu za kimkakati alizopewa wakati alipoteuliwa ili aondoe upinzani uliopo nchini, kama angekuwa amepata mkanganyiko alitakiwa kuwaita viongozi husika ili wamtafsirie katiba yao,” alisema.
        Alitoa wito kwa msajili kutambua kuwa hakuteuliwa katika nafasi hiyo kwa madhumuni ya kuanzisha malumbano ya kisiasa, na kama ataendelea na tabia hiyo ya kuchochea vyama vya siasa kazi itamshinda.
        Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alisema mvutano ndani ya vyama katika kipindi cha chaguzi ndio afya na ukuaji wa chama husika.
    Kafulila alisema kuwa mvutano unatokana na maoni na mawazo ya wanachama yenye lengo la kuboresha chama.
      “Hata Marekani vyama vya siasa vinapofikia kipindi cha uchaguzi kunakuwa na mvutano na migongano, kwahiyo kwa hapa Tanzania wananchi waelewe kuwa vyama vinapovutana ndio vinakuwa imara zaidi na wasiviingilie bali waamini kuwa demokrasia ya kweli inapatikana kwa mivutano na misuguano hadi ukweli uonekane,” alisema.
       Pia alisema kuwa kama chama hakina mvutano kitakuwa na matatizo na vinapaswa kuangaliwa kwa undani zaidi kwanini hakuna mvutano. Aliongeza kuwa demokrasia ni mvutano na kuthubutu ndio afya ya chama

Hakuna maoni