WASAKA URAIS NDANI YA CCM,WALIGAWA TAIFA SOMA HAPA UONE JINSI WALIVYOLIGAWA
Baadhi ya wanasiasa kutoka chama tawala na vyama vya upinzani, hivi sasa wamekuwa wakitumia kete ya ujana kutafuta kuungwa mkono ndani na nje ya vyama vyao.
Hata hivyo, kete hiyo inaonekana kuwachukiza baadhi ya wasomi ambao wameweka wazi kuwa kigezo cha kuwania nafasi hiyo si umri bali busara, hekima, uvumulivu na mipango makini kwa taifa.
Wanasiasa vijana wakiwemo Zitto Zubeir Kabwe, January Makamba kwa nyakati tofauti wamekuwa wakitaka mchakato wa katiba mpya utumike kushusha umri wa kuwania urais kutoka miaka 40 hadi 35.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kete ya ujana imeanza kuonekana ngazi ya kupatia madaraka kwakuwa kundi hilo lina watu wasiopungua milioni 25 sawa na asilimia 70 ya Watanzania wote.
Siasa hizo za ujana zinaelekea kuwaondoa kwenye kinyang’anyiro hicho wanasiasa nguli ambao wanatajwa kila mara kuwania urais mwakani.
Wanaobebwa na siasa za ujana ni Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, Zitto, Makamba, Dk. Hamis Kigwangala, John Mnyika na wengine wa kariba yao.
Siasa hizo pia zinatajwa kuwaondoa wanasiasa wakongwe kama Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA), Profesa Ibrahimu Lipumba (CUF), Samuel Sitta, Edward Lowassa, Benard Membe, Stephen Wassira na Fredrick Sumaye wote kutoka CCM.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamedokeza kuwa siasa hizo za ujana ndizo zilizomfanya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1995 kumkataa Rais Jakaya Kikwete, akidai bado hajakomaa vizuri kushikilia wadhifa huo.
Hata hivyo, karata hiyo ilitumiwa tena mwaka 2005 na kundi la wanamtandao lililokuwa likimpigia debe Kikwete ambaye alifanikiwa kuingia Ikulu kwa ushindi waliouita wa ‘Tstunami’.
Tayari Makamba, ametangaza nia ya kuwania urais huku akiweka wazi kuwa rais ajaye anapaswa kutoka katika kundi la vijana wanaohimili changamoto za wakati tofauti na wazee.
Kauli hiyo imeungwa mkono na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, aliyekaririwa na chombo kimoja cha habari kuwa vijana wanapaswa kushika hatamu.
Warioba alikaririwa kuwa hategemei kuona majina ya ‘wazee’ wenzake kama Dk. Salim Ahmed Salim katika kinyang’anyiro hicho bali vijana aliowaita wana fikra mpya.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili waliweka wazi kuwa kutumia kigezo cha ujana kuwania nafasi hiyo ni kuonyesha upeo mdogo.
Akizungumzia hilo, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Profesa Mwesiga Baregu, alisema ujana hauwezi kuwa kigezo namba moja cha kumpata rais anayefaa kumrithi Kikwete.
Alisema umri hauwezi kuwa sifa ya kwanza kwa kiongozi anayefaa kuwa rais ajaye, bali muhimu ni kumpima mtu kwa hekima, upendo wake kwa watu, uadilifu, umakini, uzalendo, kukubali kuwa mtumishi wa watu na afya njema.
Profesa Baregu alisema kuwa wapo viongozi wengi wenye umri mkubwa na wanafanya vizuri katika nafasi ya urais kama vile Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye amefanya kazi nzuri katika usimamizi wa ardhi ya nchi yake.
“Kama atatokea kiongozi akapata nafasi hiyo akiwa na umri mkubwa, anatakiwa kusikiliza ushauri wa vijana na kama kijana akipata nafasi hiyo pia anatakiwa asikilize ushauri wa watu wazima,” alisema Profesa Baregu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk. Benson Bana, alipinga hilo na kusema kuwa hakuna mahali popote katika katiba ya nchi panapoonyesha kwamba ujana ni kigezo tosha kwa mtu kuwa rais.
Alisema kuwa kigezo cha ujana hakitajwi mahali popote katika katiba ya nchi au chama chochote cha siasa kuwa miongoni mwa sifa za mtu anayefaa kuwa rais wa Tanzania.
Alizitaja baadhi ya sifa zinazostahili kuwania urais kuwa ni mtu kuwa mzalendo, kuheshimu taasisi ya urais, kutokuwa fisadi, kula rushwa, mtu mwenye uwezo wa kulinda tunu za taifa na mwenye elimu inayokubalika kikatiba.
“Sifa nyingi zimekuwa zikitajwa na viongozi waliotangulia kama Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na mpaka sasa hakuna kigezo cha kisayansi kinachothibitisha kwamba kijana anafaa kuwa rais katika taifa lolote na mtu mzima hafai,” alisema Dk. Bana.
Alitoa onyo na kuwataka wale wanaotumia kigezo hicho, kuacha kuwapotosha Watanzania kwa kujificha katika kigezo hicho cha umri kujihalalishia nafasi hiyo ya urais.
Dk. Bana alitoa wito kwa wale wenye nia ya kugombea urais, kwamba wanachotakiwa kufanya ni kueleza mambo wanayofikiria kulifanyia taifa na si kuegemea katika kivuli cha ujana.
Aliwataka Watanzania kuwa makini na viongozi wanaojitangaza kutaka nafasi hizo na badala yake waache watu wawainue na kuwatangaza kuwa wanafaa.
Mbunge mstaafu wa Muleba Kaskazini, Ndimara Tegambwage, alisema kuwa kigezo cha ujana si hoja inayotosheleza kumpata rais anayefaa kuongoza taif .
Alisema mtu anayezungumzia ujana wa umri ana tatizo kwani ujana wa kiongozi anayefaa ni yule mwenye uwezo wa kiakili, kufikiri, kuthubutu na hekima.
“Kama ujana unaozungumzwa ni wa umri wa miaka 20 au 40 si hoja, wala ujana wa uporaji wa mabilioni ya fedha kutoka Benki Kuu na kujimilikisha mwenyewe kwangu si kigezo cha urais,” alisema Tegambwage.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, alisema kuwa sifa ya ujana pekee haitoshi kumuwezesha mtu kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumzia kuhusu kauli iliyotolewa na Jaji mstaafu Joseph Warioba ya kuwaunga mkono vijana kugombea urais na kuwataka wazee kuwapisha katika uchaguzi mkuu ujao, Nape alisema hawezi kupinga wazo lake kwa kuwa anao uhuru kikatiba wa kutoa mawazo kama Mtanzania mwingine.
Nape alisema kuwa pamoja na mawazo yake, lakini ujana pekee haiwezi kuwa sifa inayotosha kupatikana kwa rais wa nchi hii bali zinatakiwa sifa nyingine za ziada.
“Umri si kigezo tosha kwa mtu kuwa kiongozi, upo ushahidi unaoonyesha kulikuwa na baadhi ya vijana ambao walipewa nafasi na waliharibu na wapo watu wazima waliopewa nafasi na waliharibu pia, hivyo umri kwangu si kigezo,” alisema Nape.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema kuwa kwake suala la umri halioni kama lina tija.
Mtatiro alisema kuwa sifa anazotakiwa kuwa nazo rais wa nchi ni zile zilizowahi kutajwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1995 za uadilifu, uwajibikaji, uwezo wa kutetea na kulinda katiba ya nchi.
“Umri kwangu si kigezo kwani wapo viongozi wengi wenye umri mkubwa wa miaka 70 hadi 80 wanaofanya vizuri katika nchi zao, na pia wapo vijana walioingia katika madaraka wakiwa na miaka 26 kama vile Joseph Kabila wa DRC,” alisema Mtatiro.
Alisema kuwa kama kuna mtu anayeamini anaweza kulinda katiba ya nchi anafaa kuwa rais ajaye bila kujali umri wake.
Chanzo ni Gazeti Makini la Tanzania Daima
Hakuna maoni
Chapisha Maoni