JUMLA YA WANANCHI 180 WAKAMATWA DAR NA KUSWEKWA RUMANDE, 400 WATOZWA FAINI KISA NI BODABODA, ZAIDI SOMA HAPA
KUNA
vijana waendesha bodaboda 180 waliokamatwa jijini Dar es Salaam na sasa
wapo mahabusu, imedaiwa. Wengine 400 wametozwa faini na wengine
wamehukumiwa kwa kosa la kuingiza bodaboda katikati ya Jiji.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati ya Madereva wa Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, Daudi Laurian.(Martha Magessa)
Alisema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Laurian aliiomba Serikali kuwaachia huru madereva wote wa bodaboda,
waliokamatwa kwa kosa la kuingiza bodaboda katikati ya Jiji.
“ Mpaka
sasa kuna vijana 180 waliokamatwa na wapo mahabusu na wengine 400
wametozwa faini mpaka sasa na wengine wanahukumiwa kwa kosa hili,”
alidai.
Alisema
agizo hilo la kutoingia mjini, limesababisha mambo mengi, ikiwemo
madereva kuishi kwa hofu ndani ya nchi na madereva kutozwa faini ya
fedha nyingi, ambazo ni Sh 50,000, Sh 100,000, Sh 250,000 na Sh 450,000.
Alisema
fedha hizo ni nyingi na zinazidi uwezo wa vipato vya madereva hao na
zinakinzana na Kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchikavu
na Majini (Sumatra).
“Fedha
hizi zinatozwa, lakini wakati mwingine madereva bodaboda hawapatiwi
risiti; na wakati mwingine wanapatiwa risiti feki” alidai Laurian.
Pia,
alisema wanaomba agizo hilo la Serikali la kupiga marufuku bodaboda
kuingia katikati ya Jiji, lisitishwe, kwani sababu iliyotolewa na Mkuu
wa Mkoa, Said Meck Sadiki, kuwa bodaboda zinasababisha ujambazi, si za
kweli.
Alidai kuwa bodaboda ambazo hazipo kisheria, ndizo zinahusika na matukio hayo ya ujambazi ; na sio bodaboda za kibiashara.
Alisema
ili kudhibiti uhalifu na utoaji wa huduma bora, wilaya zote tatu za
Ilala, Temeke na Kinondoni, zina alama za utambulisho wa kimaeneo kwa
mujibu wa Kanuni za Sumatra, ambapo Wilaya ya Temeke ni rangi ya Kijani,
Ilala rangi Nyekundu na Kinondoni rangi ya Bluu.
Aliomba
Serikali kutoa ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo ili kulinda ajira za
vijana wengi, ambao kipato chao kinategemea bodaboda.
Gazeti
hili lilijaribu kuwasiliana kwa simu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,
Marietha Minangi, kutokana na madereva wengi waliokamatwa na kuwekwa
mahabusu, wapo katika eneo lake la Ilala. Mtu mmoja aliyeshika simu ya
Kamanda huyo, alijibu kwa kifupi kuwa “ Nimesikia shida yako,
nitamwambia yeye”.
Gazeti
hili halikuishia hapo, bali liliwasiliana kwa simu na Kamanda wa Kanda
Maalumu ya Polisi ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kutokana na polisi wa
kanda hiyo, ndio waliokamata na wanaendelea kukamata vijana hao
waendesha bodaboda.
Kova
alisema kwanza hana taarifa kama waendesha bodaboda, walifanya mkutano
wao na waandishi wa habari jana. Pili, Kova alisema hawezi kutoa taarifa
ya idadi ya waendesha bodaboda, waliokwishakamatwa na waliopo mahabusu,
kwa sababu anayejua hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye ndiye
aliyetoa agizo hilo la bodaboda.
Alisisitiza
kuwa Mkuu wa Mkoa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Mkoa na ndiye Msemaji wa suala hilo. Kova alisema Jeshi la Polisi,
Halmashauri ya Jiji na halmashauri za manispaa ni watekelezaji tu wa
agizo hilo la Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
“Aliyetoa
agizo juu ya bodaboda ni Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati
ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa. Mimi siwezi kutoa taarifa juu ya suala
hilo. Jeshi la Polisi na Halmashauri ya Jiji tunatekeleza tu agizo hilo.
Mtafute Mkuu wa Mkoa umuulize,” alisema Kova saa 11.45 jana jioni.
Aidha,
gazeti hili lilijaribu kuwasiliana mara mbili kwa njia ya simu na Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki. Alipopokea simu kwa mara ya
kwanza, gazeti lilimweleza kuhusu malalamiko hayo ya madereva wa
bodaboda na kumuomba atoe ufafanuzi.
Mkuu wa
Mkoa aliomba apigiwe baadaye kwa maelezo kuwa yupo hospitali.
Alipopigiwa mara ya pili, alisema apigiwe baadaye kwani bado yupo
hospitali.
Maoni 1
Hi Thank' for Visit Us;
ARKA Softwares & Outsourcing is an IT Company focusing on software & Web development and providing offshore outsourcing solutions to enterprises worldwide.website development company in australia
Chapisha Maoni