TAMKO LA WANANCHI NGAZI YA JAMII (GDSS) KUHUSU BAJETI YA TAIFA 2014/2015
TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii kutoka maeneno mbali mbali ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), Kikundi Kazi cha Uchambuzi wa Bajeti (BATT) na Asasi nyingine za Kiraia tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi wa kina na kuanisha maboresho na mapungufu ya bajeti ya taifa ya 2014/15 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mh. Saada Salum Mkuya tarehe 12 Juni 2014 Bungeni Dodoma.
Kwanza tunaipongeza serikali kwa
kuonesha nia madhubuti za kukabiliana na upotevu mkubwa mapato kwa kujaribu
kurekebisha sheria mbali mbali za kodi. Pia Tunapongeza kuondolewa kwa mamlaka
ya waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi, hii ni hatua nzuri ya kuweza
kukabiliana na ufisadi, rushwa na watu wachache kunufaika na misamaha ya kodi.
Hata hivyo sehemu kubwa bajeti ya mwaka huu imeonesha mapungufu makubwa
katika mfumo mzima wa uwajibikaji wa serikali, katika ukusanyaji wa mapato na
hata mgawanyo wake. Lakini pia bajeti hii imeelekezwa zaidi kwa sekta binafsi
na wafanyabiashara wakubwa kuliko Watanzania walio wengi ambao ni wazalishaji wadogo
na walipa kodi wakubwa.
Maudhui
Bajeti imeainisha
mapato ya shilingi za Kitanzania trilioni 19.9. Kati ya fedha hizo matumizi ya
kawaida ni shilingi trilioni 13.6 (68.3%) wakati shilingi trilioni 6.3 ni
matumizi ya maendeleo sawa na (31.7%). Tumeshtushwa kuona bajeti ya maendeleo haijaongezeka
kama tulivyorajia. wakati kwa sehemu kubwa ndio tegemeo kwa maendeleo ya
Watanzania. Tunasikitika kwasababu
hakuna tofauti kubwa kati ya bajeti ya mwaka jana wa fedha 2013/2014 ambayo
matumizi ya kawaida yalikuwa Trilioni 12.6 (69.2%) na matumizi ya maendeleo
Trilioni 5.6 (30.8%).
DENI LA TAIFA
Tumeshangazwa kuona deni la taifa likiongezeka kufikia shilingi za Kitanzania trilioni 30.5 ukilinganisha na Trilioni 23.6 mwezi Machi
2013, na kuwa kubwa kuliko bajeti ya taifa huku serikali ikisema kuwa deni hili
ni himilivu. Licha ya kwamba deni
hili la taifa linazidi kukua, bado tunashangaa kuona serikali inasisitiza
kuendelea kukopa kwa kigezo cha deni kuwa himilivu na kwamba serikali
inakopesheka. Wakati huohuo Serikali inashindwa kusimamia ulinzi na mgawanyo
mzuri wa rasilimali tulizo nazo na inatoa misamaha ya kodi isio na tija kwa
taifa.. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kiasi cha shilingi trilioni 1.6
kilipotea kutokana na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija. Tunadai uwajibikaji wa serikali katika kusimamia ukusanyaji wa mapato
na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ambavyo ni endelevu.
VIPAUMBELE VYA BAJETI
Serikali imeweka vipaumbele zaidi katika sekta ambazo zipo katika mpango wa
Matokeo makubwa sasa ( Maji, Kilimo, Elimu, utawala bora na miundo mbinu).
Sekta hizi zimetengewa kiasi cha Trilioni 7.9.
Tunadai pia uendelevu wa sekta nyingine kama Afya ambayo imekua na
matatizo makubwa hasa kwenye eneo la afya ya uzazi na afya ya jamii. Tunahoji
sekta ya afya kutokua sehemu ya vipaumbele hivi
wakati wanawake na watoto hawana uhakika na upatikanaji wa huduma za afya
nchini na wanawake takribani 24 kufa kila siku kwa uzazi?
Pamoja na kupongeza kuondolewa kwa mamlaka ya waziri wa fedha kutoa
misamaha ya kodi tuna mashaka na ongezeko kubwa la misamaha ya kodi kwa mapato
yasiokuwa na mauzo ya hatifungani kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB)
katika soko la mitaji ya Tanzania ambalo wakopaji wake ni wawekezaji wakubwa,
huku wafanyabiashara wadogo wenye kipato kati ya milioni 4 hadi milioni 7 kwa
mwaka wakiongezewa mzigo mkubwa wa
ulipaji kodi. Sekta isio rasmi haikuwekewa mazingira mazuri ya ukuaji na
wakopaji wakubwa ni Wanawake, Vijana na wanaume maskini. Tunadai uwepo wa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo pamoja na
mfumo mzuri wa sekta isiyo rasmi ambayo kwa sehemu kubwa ndio kimbilio la
wanyonge.
Katika sekta ya kilimo mkazo umewekwa katika kutoa misamaha ya kodi kwenye
Matrekta ambayo yataendelea kuagizwa nchini bila ya kulipiwa ushuru. Msamaha
huu wa kodi haujatengeza mazingira ya namna ya kumnufaisha mkulima mdogo nchini
na badala yake unanufaisha wakulima wakubwa na wakodishaji wa matrekta hayo.
Jambo hili linaendeleza mfumo wa unyonyaji na ubepari kwa wakulima wadogo na kupanua wigo wa
matabaka kati ya wakulima wadogo na wakubwa. Pia mpango huu unaendeleza ulimbikizaji kiporaji
wa ardhi nchini na kuongeza migogoro isiyoisha kati ya wawekezaji na wakulima
wadogo, na wafugaji. Tunadai mgawanyo wa
ardhi uendane na mahitaji ya makundi katika maeneo husika hususani kwa
wanawake, vijana na wanaume maskini.
Serikali imeonesha juhudi za makusudi za kutaka kulinda viwanda na bidhaa
za ndani kwa kuongeza kodi kwa bidhaa ambazo zinaagizwa kutoka nje ya nchi. Tunashauri
mkakati huo huo ufanywe pia ili kuwalinda wawekezaji wadogo wanaowekeza kwenye
gesi asilia pamoja na mafuta. Hii itasaidia kuongeza tija kwa wawekezaji wadogo
katika uchimbaji pamoja na uvunaji na hatimae itasaidia kuinua pato la taifa na
kupunguza utegemezi wa kibajeti nchini.
Katika
hotuba ya bajeti serikali imesema imetoa jumla ya ajira mpya 630,616 kiwango
hiki ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya wahitimu 900,000 wanaoingia
kwenye soko la ajira kila mwaka pamoja na wale waliopo tayari. Tunahoji
ajira hizi zilizotolewa na serikali kwa mwaka 2013/2014 zinakidhi mahitaji ya
soko la ajira? Na Je ajira hizi ni salama na endelevu zinazojali utu, heshima
na staha? Bado tunadai mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa
malighafi vikubwa
na vidogo vinavyoweza kuongeza ajira kwa waliokuwa wengi vijijini na mijini.
Katika sekta ya elimu serikali
imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 500
kwa ajili ya halmashauri 80 kujenga
nyumba za walimu. Kiasi kama hiki kilitengwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014
kwa halmashauri 40 nchini. Tunahoji pesa hizo zilizotumika zilijenga nyumba
ngapi na katika halmashauri zipi na zenye ubora gani? Je upo wapi mkakati wa
ujenzi wa mabweni, kuboresha mazingira ya kufundishia na vifaa vya kujifunzia,
na mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu?
Mwisho tumesikitishwa sana kuona Waziri wa Fedha akikiri bungeni kwamba
sera zetu za kiuchumi zinatokana na mashirika makubwa ya kibeberu kama vile IMF
kupitia mpango wa Policy Support
Instrument (PSI). Hali hii inathibitisha kwamba mipango mingi iliyopo nchini
haitokani na wananchi bali matakwa ya mashirika makubwa yanayoendeleza ulimbikizaji
kiporaji wa rasilimali nchini. Lakini pia serikali inaendelea kupuuza utaalamu wa wataalamu wa uchumi wa ndani
ya nchi.
Madai
Kutokana na uchambuzi ulioainishwa hapo juu tunadai yafuatayo:
- Kuwepo mfumo shirikishi na endelevu katika kutengeneza na kufatilia utekelezaji wa bajeti ya taifa na serikali za mitaa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi, wanawake na wanaume na makundi yaliyoko pembezoniMisamaha ya kodi katika kilimo ilenge kuwanufaisha wakulima wadogo wadogo na sio wawekezaji wakubwa.
- Kukua kwa uchumi wa nchi kuende sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
- Sekta ya afya ipewe kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ili ifikie 15% ya bajeti kama ilivyoagizwa katika azimio la Abuja.
- Uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa na tija.
Tamko hili limetolewa na:
Sisi wanaharakati wa kikundi kazi cha uchambuzi wa bajeti,
wanaharakati kutoka Dar es Salaam,
Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo
(GDSS),kwa ushirikiano na TGNP Mtandao
Imesainiwa na:
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao
Tarehe 15 Juni 2014
Hakuna maoni
Chapisha Maoni