Zinazobamba

TOSCI YAWAKARIBISHA WANANCHI KUPATA ELIMU YA MATUMIZI BORA YA MBEGU MAONESHO YA SABASABA


Na Mussa Augustine 

Wananchi wameombwa kutembelea banda la Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kupata elimu kuhusu matumizi ya mbegu bora.

Rai hiyo imetolewa leo, Julai 2, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda hilo. 

Amesema taasisi hiyo, iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, ina majukumu mbalimbali, ikiwemo kusajili aina zote za mbegu zinazowafikia wananchi ili kuhakikisha zina ubora.

Aidha, Chimagu amesema matumizi ya mbegu bora husaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima.

Hivyo,taasisi hiyo inaendelea kuthibiti ubora wa mbegu ili kuhakikisha wananchi wanapata mbegu zinazoweza kulimwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.

"Mbegu yoyote ambayo ni bora lazima iwe imesajiliwa, na ili isajiliwe lazima ipitie hatua kadhaa za majaribio ili kuthibitisha kama inafaa kuzalishwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuwa na sifa zake bainishi kwa kila aina ya mbegu, iwe mahindi, mpunga au mtama," amesema Chimagu.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa kinara katika kuhamasisha kilimo biashara, huku msingi wa kilimo hicho ukiwa ni matumizi ya mbegu bora.

Ameongeza kuwa mchango wa TOSCI katika sekta ya kilimo ni kuhakikisha wakulima wanazalisha mazao kwa tija.Pia amesema TOSCI inahakikisha mazao yanayozalishwa na wakulima wa Tanzania yanakidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuchangia upatikanaji wa usalama wa chakula nchini.

"Kwa sasa Tanzania inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 130, ambao msingi wake ni matumizi ya mbegu bora.

Amesema Rais Samia ameendelea kufungua masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi, maana yake tumeitangazia dunia kuilisha,sisi kama TOSCI tunatoa elimu kwa wakulima na wadau wote kwamba, kwa sababu Serikali imehamasisha kilimo biashara, wasilime bila kujihakikishia kuwa mbegu hizo bora zimehakikiwa na TOSCI."Mbegu zote lazima ziwe kwenye kifungashio, na ni marufuku kwa mujibu wa sheria mbegu kuuzwa bila kifungashio kwa sababu inapokuwa imefungashwa, inakuwa imefuata misingi yote, na kwenye kifungashio kunakuwa na taarifa za aina ya mbegu pamoja na jina la kampuni iliyozalisha mbegu hizo," amesema.

No comments