Zinazobamba

VETA KIHONDA YAJA NA TEKNOLOJIA INAYORAHISISHA KILIMO CHA MBOGA MBOGA NA MPUNGA


Na Mussa Augustine

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kupitia Chuo Cha VETA Kihonda Morogoro imeleta ubunifu wa mashine ya kisasa ya kulimia maarufu kama(Power Tiller), iliyobuniwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya kilimo nchini ili kuwasaidia wakulima kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zinazowakabili mashambani.

Akizungumza leo, Juni 1, 2026, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkufunzi Mwandamizi wa VETA Morogoro-Kihonda, Fredrick Uliki, amesema mashine hiyo imebuniwa baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu mashine zinazoagizwa kutoka nje ya Tanzania ambazo zimeonekana kutokidhi kikamilifu mazingira ya kilimo.

"Tumefanya ubunifu wa mashine hii kutokana na utafiti tulioufanya na kubaini kuwa baadhi ya mashine zinazoagizwa kutoka nje ya Tanzania hazina uimara wa kutosha kufanya kazi kwa muda mrefu kwenye mashamba ya mabondeni na maeneo yenye milima. Hivyo, tukaja na teknolojia inayokidhi mazingira yetu," amesema Uliki.Ameongeza kuwa mashine hiyo imeundwa mahsusi kurahisisha kilimo cha mboga mboga, hususan kwa wakulima wanaolima katika maeneo ya mabondeni ambako matrekta makubwa hushindwa kufika kutokana na hali ya eneo kutofikika.

Aidha, amesema mashine hiyo pia ni muhimu kwa wakulima wa mpunga kwani husaidia kugandua ardhi na kulainisha udongo vizuri, hali inayowezesha mbegu kuota kwa haraka na kwa wingi, hivyo kuongeza uzalishaji.

Halikadhalika, mkufunzi huyo ameongeza kuwa mashine hiyo ina uwezo wa kulima eneo la hadi hekta tatu kwa siku, kutegemeana na nguvu ya mtumiaji, aina ya udongo pamoja na jiografia ya eneo husika.

Amesema kuwa katika maeneo ya tambarare, mashine hiyo huruhusu kazi kufanyika kwa kasi zaidi kuliko maeneo yenye miteremko au mabondeni.

Aidha, amesema wakulima hawatakumbana na changamoto ya upatikanaji wa vipuri vya mashine hiyo kwani vinapatikana kwa urahisi katika mikoa mbalimbali nchini na vinauzwa kwa bei nafuu, hatua inayolenga kuhakikisha mashine hiyo inakuwa suluhisho endelevu kwa sekta ya kilimo.

No comments