Zinazobamba

NLD: HATUTASHIRIKI MAANDAMANO YANAYOHAMASISHWA NA WANAHARAKATI – DOYO

Na Mussa Augustine

Chama cha National League for Democracy (NLD) kimesema hakitashiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika Julai 7, 2026, kikidai kuwa maandamano hayo ni kinyume cha sheria kwa kuwa hayajapata kibali kutoka serikalini.

Kauli hiyo imetolewa leo, Julai 1, 2026, na Katibu Mkuu wa Taifa wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, wakati wa ufunguzi wa kikao cha siku mbili cha Kamati Tendaji ya NLD. Kikao hicho kinajadili masuala mbalimbali, ikiwemo tathmini ya hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Doyo aliwataka Watanzania na wanasiasa kutoshiriki maandamano hayo, akisisitiza kuwa serikali imeyapiga marufuku."Ninawasihi Watanzania na wanasiasa wenzangu wasijitokeze kwenye maandamano yaliyotangazwa kufanyika Julai 7 kwa sababu serikali imeyakataza. Pia, Watanzania wawatazame waandaaji wa maandamano hayo kwa umakini kutokana na yaliyotokea Oktoba 29, 2025, ambayo kila Mtanzania aliyashuhudia," alisema Doyo.

Aliongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuwaepuka wanaharakati au mwanasiasa yeyote ambaye, kwa mtazamo wake, analenga kulirudisha taifa katika mazingira yasiyofaa.

Doyo alisema chama hicho hakiko tayari kuunga mkono chama chochote cha siasa au kundi lolote la wanaharakati katika shughuli ambazo, kwa mujibu wa chama hicho, zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani.

"Sisi tutasimama katika kulinda usalama wa taifa letu na usalama wa Watanzania kwa kuzingatia sheria za nchi," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa NLD, Mfaume Khamis Hassan, alisema chama hicho kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na kinaendesha shughuli zake kwa misingi ya sera na malengo yake, bila kufuata mwelekeo wa vyama vingine vya siasa.

Aidha, aliwataka wanachama wa NLD kutoshiriki maandamano hayo, huku akiwaomba Watanzania kupuuza wanasiasa na wanaharakati wanaohamasisha maandamano ambayo, kwa mtazamo wake, yanaweza kuhatarisha amani.

Mfaume alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, umeshafanyika na viongozi wamepatikana, hivyo hakuna sababu ya kuanzisha vurugu. Aliwahimiza wananchi kutokubali kurubuniwa na watu wenye nia ya kuvuruga amani na utulivu wa nchi.

No comments