ZAMBIA YAJIFUNZA UBUNIFU WA TANZANIA KATIKA MATUMIZI YA GESI ASILIA

Nchi ya Tanzania imetajwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika matumizi ya rasilimali zake za asili kuleta maendeleo jumuishi na kutoa suluhisho la nishati safi kuanzia mijini hadi vijijini.
Hayo yamebainishwa leo Juni 27, 2026 na ujumbe kutoka Zambia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Zambia, Mha. Alex Simwaba, ulipotembelea Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Kinyerezi II pamoja na Kituo cha Kusambaza Gesi cha Kinyerezi kwa lengo la kujifunza namna Tanzania inavyotumia rasilimali zake za asili kuleta maendeleo, hususan katika uzalishaji wa umeme na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mha. Simwaba amesema inavutia kuona namna Tanzania inavyotumia gesi asilia katika matumizi mbalimbali ikiwemo kwenye magari, viwandani na sekta nyingine muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi, pamoja na uzalishaji wa umeme.
"Gesi hii asilia ni mbadala mzuri sana wa mkaa ambao kwa miaka mingi umesababisha changamoto za ukataji miti na uharibifu wa mazingira," amesema Mha. Simwaba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vituo vya Kuzalisha Umeme kwa Mafuta na Gesi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Marco Zacharia, amesema ziara hiyo imekuwa fursa ya kipekee ya kubadilishana ujuzi kati ya Tanzania na Zambia.
Amesema nchi hizo mbili zitaendelea kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, huku akibainisha kuwa wataalamu wa Tanzania wamealikwa kwenda Zambia kujifunza namna uzalishaji wa umeme kwa kutumia makaa ya mawe unavyofanyika.
Ameongeza kuwa, katika kufanikisha lengo la Tanzania la kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, ni muhimu kuendelea kujifunza na kubadilishana uzoefu na mataifa mbalimbali, hususan nchi jirani kama Zambia.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya kidiplomasia yanayowezesha mataifa mbalimbali kuja nchini kujifunza mafanikio ya Tanzania katika sekta ya nishati.


No comments
Post a Comment