Zinazobamba

VETA Dakawa Yaja na Teknolojia Mpya ya Kuvunia Sumu ya Nyuki


Na Mussa Augustine

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kupitia Chuo Cha VETA Dakawa imeleta ubunifu wa mzinga wa nyuki wa kisasa pamoja na mashine ya kuvunia sumu ya nyuki kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu fursa za ufugaji wa nyuki kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Akizungumzia ubunifu huo, Mkufunzi kutoka VETA Dakawa, Theodora Kiyungu, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na misitu mingi inayofaa kwa shughuli za ufugaji wa nyuki, jambo linalotoa fursa kubwa za uzalishaji wa mazao mbalimbali yatokanayo na nyuki, ikiwemo sumu ya nyuki inayotumika kutengeneza dawa za binadamu.

"Mzinga huu umeunganishwa na kifaa maalumu kinachotumia umeme wa kuchaji kwa ajili ya kuvuna sumu ya nyuki. Kifaa hiki kina paneli na sehemu ya kioo yenye nyaya zinazopitisha umeme wa volti 10, ambazo huwekwa katika mlango wa mzinga," amesema Bi. Kiyungu.

Ameongeza kuwa, "Nyuki anaporudi kutoka kutafuta chakula hugusa nyaya hizo na kupata shoti ndogo isiyomdhuru, hali inayochochea utoaji wa sumu ambayo hukusanywa kwa ajili ya kuvunwa."Kiyungu ameongeza kuwa kifaa hicho huwekwa kwenye mzinga kwa muda wa nusu saa, kisha hutolewa na sumu ya nyuki huvunwa.

Kwa mujibu wa mkufunzi huyo, sumu ya nyuki ni zao lenye thamani kubwa kwani hutumika kutengeneza dawa zinazotumika hospitalini pamoja na vipodozi. Hivyo, ni fursa muhimu ya kuongeza kipato kwa wafugaji wa nyuki.

Amefafanua kuwa VETA Dakawa imeamua kutumia Maonesho ya Sabasaba kutoa elimu hiyo baada ya kubaini kuwa wafugaji wengi wamekuwa wakijikita katika mazao mawili pekee ya nyuki, ambayo ni asali na nta, huku wakisahau mazao mengine yenye thamani kubwa kiuchumi, ikiwemo sumu ya ny

Hata hivyo, amewashauri wananchi kujifunza ufugaji wa nyuki kupitia VETA Dakawa, akibainisha kuwa chuo hicho kwa sasa kinatoa pia kozi ya ufugaji wa nyuki kwa njia ya mtandao ili kuwafikia watu wengi zaidi.

"Mimi, Theodora Kiyungu, nimefanya ubunifu wa mzinga huu, halafu mashine ya kuvunia sumu ya nyuki imebuniwa na mtaalamu mwingine," amesema Kiyungu.



No comments