Zinazobamba

TOST ITAKUWA SEHEMU MUHIMU KATIKA UTEKELEZAJI WA DIRA YA 2050

Yawaomba wafanyabiashara na wawekezaji kulipa kodi kwa hiari.

Na Mussa Augustine

Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) imesema kuwa itakuwa sehemu muhimu katika utekelezaji wa Dira ya 2050 kwa kuhakikisha inawasaidia wafanyabiashara na wawekezaji wanapokumbana na vikwazo vya kikodi.

Hayo yamesemwa leo, Julai 2, 2026, na Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la taasisi hiyo lililopo kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba).

Aidha, Mtui amesema kuwa moja ya malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kumpa ujasiri mfanyabiashara au mwekezaji ajue kwamba anapokutana na vikwazo vya kodi, kuna taasisi inayoweza kutoa suluhu ya vikwazo hivyo.

"Kodi ni jambo muhimu sana katika kuendesha nchi. Kwa hiyo, tunawaasa walipa kodi walipe kodi zao vizuri, na pale wanapokutana na vikwazo, tupo kwa ajili ya kuondoa vikwazo hivyo ili waweze kulipa kodi zao kwa hiari," amesema Mtui.Aidha, amesema kuwa wao kama Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi watakuwa sehemu muhimu sana katika utekelezaji wa Dira ya 2050.

Amesema kuwa ili Dira ya 2050 iweze kufikiwa, ni lazima mazingira ya biashara na uwekezaji yaboreshwe.

"Tunaangalia uchumi wa nchi hii ukue kwa wastani usiopungua asilimia 10 ili kufikia malengo tunayotazamia ya dola trilioni 1. Sasa ukuaji huo unahitaji mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

Na sisi kama Taasisi ya Kushughulikia Malalamiko ya Kodi tutakuwa kama kiungo cha kuhakikisha kwamba pale inapotokea msuguano tunaweza kuutatua kwa wakati na kuboresha mazingira hayo ili watu wafanye biashara zao, wakue kibiashara, na walipe kodi zao kwa usahihi na kwa hiari."

No comments