WANANCHI KATA YA MAKURUMLA WALILIA MAJI.

"Wadai hawajapata Maji kwa muda mrefu,huku Mamlaka zikishindwa kuchukua hatua haraka.
"Wadai kutumia gharama kubwa kufuata Maji maeneo jirani.
Na Mwandishi Wetu.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Wilaya ya Ubungo Henry Mwenge ameitaka Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Dar es salaam(DAWASA)kushughulikia kwa haraka kero ya Maji inayowakumba Wananchi wa kata ya Makurumla Manispaa ya Ubungo.
Mwenge ametoa agizo hilo leo Machi 11,2026 jijini Dar es salaam wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kata ya Makurumula iliyowasilishwa na diwani wa kata hiyo Bakari Kimwaga,kwenye kikao maalumu cha Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya kata hiyo.
Amesema kuwa DAWASA inapaswa kuchukua hatua za haraka kwani changamoto hiyo imekua ya muda mrefu nakwamba Wananchi wa kata hiyo wanaishi bila maji jambo ambalo linahatarisha maisha yao.
"Pamoja na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Elimu na Miundombinu ya barabara za ndani katika kata ya Makurumla,lakini bado tuna changamoto kubwa ya Maji,kwenye hili lazima tuseme na wenzetu wa DAWASA mtatuvumilia,suala hili halina majadiliano (discussion),
yaani hakuna mbadala wa maji,suala la maji linagusa maisha ya kila mtu,maji ni uhai na hatuna njia nyingine zaidi ya maji,kwahiyo mwananchi akikosa maji lazima alalamike." amesema Mwenge
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Makurumla Bakari Kimwaga amesema kuwa kumekuwepo na wizi wa maji unaofanywa na baadhi ya watu(Vishoka) hivyo uongozi wa kata hiyo umeanza kushirikiana na DAWASA kudhibiti mfumo huo.
"Kwanza kuhusiana na wizi wa maji kwa kutumia mfumo wanaita"mfumo wa nyoka"tunaendelea kushirikiana na wenzetu DAWASA,na hata ukiangalia ripoti kwa mwezi uliopita tumeweza kukamata baadhi ya watu ambao walikua wakipitisha hiyo mipira na wametozwa faini nzuri tu,lakini wengine walishindwa kulipa na wapo ndani(mahabusu)hadi sasa"amesema
Nakuongeza kuwa"kuna changamoto nyingine ambayo baadhi ya watu wanapata maji huku wengine wakikosa,inahitajika kuwepo kwa haki sawa katika kupata huduma ya maji kama ilivyo katika nishati ya umeme.
Nae Liberatha Mduga mkazi wa Makurumla amesema kwamba kero kubwa wanayoipata ni ukosefu wa maji ambapo amebainisha kwamba mara ya mwisho kupata maji hayo ni mwaka jana, na wanachoshangazwa ni kuona maofisa wa DAWASA wanaendelea kwenda kusoma mita za maji ambazo zinaonesha sifuri.
"Tumejaribu kufuatilia lakini hakuna majibu ya kuridhisha,na huo mgao wa maji ambao tulitarajia kuweza kupata, mpaka leo hatujafanikiwa kupata,hivyo tunamuomba Waziri wa Maji atuone wananchi wa kata ya Makurumula,
kwasababu tunateseka hasa sisi wanawake tunabeba maji kutoka maeneo ya mbali na kutumia gharama kubwa,tunanunua maji ndoo shilingi 500/= hadi 1000/= amesema.
Halikadhalika Job Mwakajumba mkazi wa Mtaa wa kwajongo amesema kuwa wanapata adha kubwa kutokana na ukosefu wa Maji licha ya kuchimbwa kisima mtaani hapo lakini Maji yalipatikana kwa siku moja tu na hadi leo hayajatoka tena.
"Wananchi wanalalmika sana kuhusu suala la maji katika Mtaa wa kwajongo,lakini ukienda Mtaa wa pili unaitwa Mtaa wa Kagera maji yanatoka,imekua ni usumbufu mkubwa sana wa Maji hususani wakina mama."amesema
Nakuongeza"tulipangiwa siku tukakubaliana Maji yatoke kwa wiki mara tatu yaani jumatatu,jumanne na jumatano,lakini toka jumatatu hadi leo jumatano hakuna Maji yaliyotoka sasa tunakwendaje hivi?amehoji Mwakajumba.


No comments
Post a Comment