Zinazobamba

TISEZA YAJA NA ZA UWEKAZAJI SEKTA MADINI BUZWAGI


Na Richard Mrusha 

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum (TISEZA) imetangaza rasmi fursa za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia eneo maalum la Buzwagi lililoko Kanda ya Ziwa. Ofisa Uwekezaji Mkuu wa Kanda hiyo, Erastus Malai, amesema eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 1,333 limetengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za uchenjuaji madini.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza fursa hizo, Malai alisema eneo la Buzwagi limeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wawekezaji ili kuhakikisha mchakato wa kuwekeza unakuwa rahisi na wa haraka. 

"Tumeweka miundombinu yote muhimu, kuanzia barabara, majengo, ofisi hadi uwanja wa ndege. 

Mwekezaji akifika hatalazimika kugharamia miundombinu, isipokuwa kuwekeza moja kwa moja kwenye kiwanda cha uchenjuaji madini," alisema.

Mbali na Buzwagi, TISEZA pia imetenga maeneo mengine maalum nchini kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Malai alitaja maeneo hayo kuwa ni Nara mkoani Dodoma lenye ekari 607, Wara Kibaha mkoani Pwani lenye ekari 100 na Bagamoyo lenye ekari 151."Maeneo haya yametengwa kwa uwekezaji kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba, magari na boti, bidhaa za ngozi, nguo, makazi na vifaa vya majumbani," aliongeza.

Aidha, Malai alibainisha kuwa uzinduzi wa maeneo hayo ni hatua mpya kwa mamlaka hiyo katika kukuza sekta ya uwekezaji nchini. Alisema mpango huo unalenga si tu kuendeleza sekta ya madini, bali pia kutoa fursa za kiuchumi kwenye nyanja nyingine muhimu.

Kwa mujibu wa Malai, fursa nyingine zilizoko Kanda ya Ziwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta za kilimo, uvuvi, utalii, ujenzi wa majengo ya biashara na ufugaji. "Tunaamini maeneo haya yatakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa taifa na ajira kwa wananchi," alisema.

TISEZA imesisitiza kuwa serikali ipo tayari kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji watakaowekeza kwenye maeneo hayo, hususan eneo maalum la Buzwagi. Vivutio hivyo vinatarajiwa kuongeza mvuto wa uwekezaji na kuhakikisha mwekezaji anapata unafuu wa gharama.

Katika wito wake, Malai amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hizo. "Tunawaalika wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza. Fursa hizi ni za kipekee na zimewekewa mazingira rafiki na salama," alisema.

Uwekezaji kwenye maeneo maalum kama haya unatarajiwa kuongeza thamani ya maliasili, kukuza viwanda, kuimarisha uchumi wa taifa na kuendeleza ajenda ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Hatua hii pia inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

No comments