TARURA GEITA WASHIRIKI KIMAONESHO YA KIMATAIFA YA MADINI KUBORESHA BARABARA ZA WILAYA
Geita, Tanzania –
Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) tawi la Geita umeshiriki katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Madini kwa lengo la kuelimisha umma juu ya kazi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kusimamia mtandao wa barabara za wilaya.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TARURA Geita, David Msechu, alisema kuwa taasisi hiyo inahakikisha ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za wilaya ili kusaidia ukuaji wa uchumi na huduma za jamii.
“Kwa sasa, TARURA inasimamia mtandao wa barabara wa kilomita 100,044 nchini kote, huku mkoa wa Geita ukihudumiwa na mtandao wenye urefu wa kilomita 7,264, ambao unapitika kwa asilimia 60,” alisema Msechu.
Aliongeza kuwa kati ya mtandao huo, kilomita 564 ni barabara zinazohudumia maeneo ya madini.“Tunaendelea kushirikiana na wadau wa madini kuhakikisha barabara hizi zinaboresha upatikanaji wa malighafi na huduma za kijamii, huku tukitenga fedha maalum kwa ajili ya miradi ya matengenezo,” alisema.
Kwa mujibu wa Msechu, kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, TARURA imetenga shilingi milioni 580 kwa ajili ya kukamilisha kilomita 210 za barabara zinazohudumia maeneo ya madini, huku baadhi ya kazi zikiwa zimekamilika na zingine zikiendelea.
Sambamba na hilo, TARURA Geita ina maabara ya kisasa ya kupima ubora wa barabara, ambayo inahudumia miradi mbalimbali ya ujenzi, umwagiliaji, miradi ya TANESCO, na miradi ya Ruwasa.
“Tuna miradi ya lami yenye urefu wa kilomita 17, ujenzi wa stendi, na madaraja kadhaa, yote yakitumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha ubora,” alisema Msechu.
Aliwataka wananchi na wadau wa madini kushirikiana ili kuepuka kuharibika kwa barabara kutokana na mizigo mizito isiyozidi viwango vinavyoruhusiwa.Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi TARURA kutoka Makao Makuu, Faiza Mbande, alisema kuwa taasisi hiyo pia inatoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya barabara.
“Tunawaelimisha wananchi kuepuka kupitisha wanyama barabarani, kulima pembezoni mwa barabara, na usafirishaji wa mizigo mizito, pamoja na kuwashirikisha kuhusu masuala ya fidia,” alisema Mbande. Aliongeza kuwa TARURA inakuza vikundi vya wananchi kwa ajili ya matengenezo madogo ya barabara na ulinzi wake.
Mbande pia alibainisha kuwa kupitia mradi wa Benki ya Dunia, TARURA itatekeleza ujenzi wa barabara za kilomita 59 katika Wilaya ya Mbongwe, zikiwemo Nyasumbwem, Mkweni, Nyomola, na Kiseka Isega, ambapo barabara tatu tayari usanifu wake umekamilika na mchakato wa kumpata mkandarasi unaendelea.
Halmashauri 135 tayari zimekuwa wanufaika na miradi hii ikiwemo wilaya za Geita, Nyang’hwale, na Bukombe.
No comments
Post a Comment