Zinazobamba

SOTTA MINING KUENDELEA NA UJENZI WA MGODI WA DHAHABU NYANZAGA, WANANCHI KUPATA MAKAZI MAPYA

Geita, Tanzania – Septemba 2025:

Sotta Mining Corporation Ltd imetangaza kuendelea na mradi wa ujenzi wa mgodi wa dhahabu wa Nyanzaga wilayani Sengerema, mkoani Geita, ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili na kuanza uzalishaji wa kwanza wa dhahabu ifikapo Januari 2027.

Akizungumza katika maonesho ya madini mkoani Geita, Mhandisi Richard Ojendo, Mhandisi Msimamizi wa Mradi kutoka Sotta Mining Corporation Ltd, alisema, ujenzi huo unahusisha pia kinu cha kisasa cha kusaga na kusafisha dhahabu. Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia kati ya Sotta Mining (80%) na Serikali ya Tanzania (20%).

Tayari kampuni imekamilisha ujenzi wa nyumba 151 za wananchi waliopisha eneo la mradi, huku nyumba nyingine 111 zikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi na zinatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.Wananchi wamenufaika pia kupitia ajira za muda mfupi na mrefu zinazotolewa na kampuni, ambapo wazawa wanapewa kipaumbele. Prisca Mapembe, mmoja wa waliojengewa nyumba, alisema: “Tumepewa nyumba bora zenye maji, umeme na visima. Pia tunapewa kipaumbele tunapojitokeza kwenye nafasi za ajira.”

Aidha, Felician Bukwimba, kijana anayejihusisha na kazi za utengenezaji tofali, alisema: “Kuwa karibu na mgodi huu ni fursa. Wazawa tunapewa ajira na hii imetuboresha kimaisha.”Mradi wa Nyanzaga unatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya serikali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya ya Sengerema na mkoa wa Geita kwa ujumla.





No comments