BoT yaendeleea na mpango wa ununuzi wa Dhahabu
Afisa kutoka Idara ya Masoko ya Fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Rehema Kassim amesema kuwa moja ya majukumu muhimu ya idara hiyo ni kuhakikisha ukusanyaji wa dhahabu kutoka kwa wachimbaji nchini, kwa lengo la kuiwezesha BoT kuongeza akiba ya fedha za kigeni.
Rehema, amesema mnamo Oktoba mwaka jana, BoT iliweka mpango mkakati wa ununuzi wa dhahabu, wenye lengo la kuwapa fursa wachimbaji wakubwa na wadogo kuuza dhahabu yao moja kwa moja kwa Benki Kuu kwa bei ya ushindani ya kimataifa.
Amesema Mpango huu pia unazingatia masharti ya Sheria ya Madini, kifungu cha 59, kinachoelekeza kuwa kila mchimbaji mwenye leseni anapaswa kuuza asilimia 20 ya dhahabu yake kwa BoT.Katika kuweka motisha kwa wachimbaji, BoT imepunguza baadhi ya tozo. Rehema ameeleza kuwa malipo ya mrabaha yameshushwa kutoka asilimia 6 hadi asilimia 4, na ada ya mauzo iliyokuwa asilimia 1 sasa imeondolewa kabisa hii imeongeza hamasa kwa wachimbaji kuuza dhahabu yao kupitia mfumo rasmi wa Serikali.
Aidha, wachimbaji hawalazimiki kuuza tu asilimia 20 pekee, bali wanaruhusiwa kuuza hadi asilimia 100 ya dhahabu yao kwa BoT, iwapo watapenda.
Kwa sasa, uchimbaji wa dhahabu unafanyika kwa ushirikiano na kampuni za uchenjuaji (refineries) ambapo BoT imeingia mikataba na kampuni tatu kuu za uchenjuaji wa dhahabu: Geita Gold Refinery (GGR) ya Geita, Mwanza Precious Metals Refinery, na Isographica Refinery ya Dodoma. Kampuni hizi huchakata dhahabu kutoka kwa wachimbaji kabla ya kusambazwa kwa BoT, kulingana na ukaribu wa eneo la uchimbaji.Kwa upande wake, Meneja wa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa BoT, Vicky Msina, amesema kuwa ushiriki wa BoT katika maonesho haya unalenga kutoa elimu kwa wananchi juu ya majukumu ya Benki Kuu, hasa katika kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni. Amesema BoT ni mdau mkubwa wa sekta ya uchumi, na moja ya njia wanazotumia kuhakikisha Serikali inapata fedha za kigeni ni kununua dhahabu, ambayo inatumika kuongeza akiba ya taifa na kuchochea maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.
No comments
Post a Comment