Zinazobamba

MWIRU KUWEKA BOMBA LA GESI KILA KATA.


*Lengo ni kuwawezesha kujaza gesi kwa urahisi.

*Asisitiza mageuzi makubwa ya kiuchumi Mkoani humo.

*Kuanzisha mashirika matatu yatakayoshindana kuzalisha Nishati ya umeme.

Na Mussa Augustine.Mtwara.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Wakulima (AAFP)Kunje Ngombale Mwiru amesema kuwa endapo Wananchi watampa ridhaa ataweka bomba la gesi kwenye kila kata,ili wananchi waweze kujaza gesi pindi wanapoishiwa kwenye mitungi yao.

Mheshimiwa Mwiru amesema hayo Septemba 25,2025 Masasi Mkoani Mtwara akiwa katika Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara wakati wa kampeni zinazoendelea Mkoani humo nakusema kuwa Mkoa huo umekua na  changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo kukatika kwa umeme na Maji pamoja na miundombinu mibovu ya barabara.
"Ndugu zangu Serikali ya CCM imeleta mpango wa kugawa mitungi ya gesi,hivi mliwauliza gesi ikiisha mtaweka wapi?... wanakuja na mitungi ya gesi wanajifanya wao wana huruma,nawaahidi kila kata nitaweka bomba la gesi watu wenye mitungi yao wakajaze pale."

Nakuongeza"Naamini wengine toka waletewe mitungi gesi imeisha hawajatumia mpaka leo,nchi gani hii wanaleta mitungi ya gesi lakini pakujaza gesi hakuna,na gesi tumekalia wenyewe hapahapa kusini,gesi hii kama ingekua inatoka Ulaya kweli,lakini gesi ipo katika Taifa  letu,tena gesi ipo kusini huo ni uongo."
Aidha amefafanua kua mabomba hayo yatakua na usimamizi maalumu ambapo Mwananchi akimaliza gesi ataenda kwa Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa atapewa karatasi ya utambulisho wa kwenda kujaza gesi hiyo nakwamba hatua hiyo inawezekana kutokana na Tanzania kua na utajiri mkubwa wa rasilimali mbalimbali ikiwemo gesi na Madini.

Aidha amesema kuwa Serikali yake itaweka ushindani wa mashirika matatu ya kuzalisha Nishati ya umeme kwani shirika la Ugavi wa Umeme Nchini(TANESCO)limeshindwa kukidhi haja ya  kuwahudumia Watanzania,ndio maana nishati ya umeme katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mikoa ya kusini imekua changamoto kubwa.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Mwiru ameendelea kutoa ahadi zake za kuwainua wakulima wa Korosho,Mbaazi na Ufuta Mkoani Mtwara,ambapo ameahidi kujenga soko kubwa la kanda ya kusini karibu na bandari ili wakulima wauze mazao yao moja kwa moja bila kupitia kwenye vyama vya  ushirika kwa mamdai kuwa vinawanyonya wakulima hao nakuchelewesha malipo kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.

Serikali yangu "Nitajenga soko kubwa karibu na bandari ambapo nitaweka majengo nitakayoyaita majina ya mazao husika,kutakua na mtaa wa Korosho,mtaa wa mbaazi na mtaa ufuta,ambapo korosho mtauza elfu kumi(10,000)kwa kilo moja,mbaazi elfu tano(5000)kwa kilo moja,na nitaweka Malori maalumu ya kusafirisha mazao yenu bure hadi Sokoni"amesema Mwiru.
Nae Mgombea Mwenza Chum Abdallah Juma amewaomba Wananchi hususani wakina mama kukichagua chama hicho ili kiweze kuwaboreshea miundombinu mbalimbali kwenye sekta ya Afya,Elimu,Masoko,kilimo, Maji,pamoja na Barabara,nakuufanya Mkoa wa Mtwara kupiga hatua kubwa kimaendeleo kwani ni Mkoa wenye utajiri mkubwa kwa kanda ya kusini.

Awali Katibu Mkuu wa Chama hicho Rashid Rai aliwaomba Wananchi wakichague chama hicho kwani kina dhamira kubwa ya kuwaletea maendeleo Watanzania hususani wakulima ambao tangu enzi za uhuru wameonekana hawana thamani huku wakifanya kazi kubwa ya kulitambulisha Taifa na Dunia kwa ujumla kupitia Kilimo.
"Hichi chama nichakwenu,tuchaguane ili tuzungumze lugha moja, sisi ni wakulima wenzenu,tumewaletea mgombea ambaye tumemtathimini anaweza kuwaletea maendeleo wakulima,hivyo nawaomba sana tarehe 29 mwaka huu pigeni kura za ndio kwa Mgombea urais Kunje Ngombale Mwiru pamoja na mgombea mwenza Chum Abdalah Juma, na Wabunge wote wa AAFP" amesema Rai.




No comments