DOYO: MIAKA 64 YA UHURU, SHULE ZINAENDELEA KUKOSA MAJI, KAMA SERIKALI IMESHINDWA KUPELEKA MAJI CHOONI, ITAWEZA NINI?
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, akiwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza, amewaeleza wananchi kuwa changamoto zinazowakabili wakazi wa Kanda ya Ziwa zinafanana katika maeneo mengi, ikiwemo matatizo ya maji, afya, ajira na barabara.
Akitoa mfano, Mhe. Doyo alisema kuwa akiwa wilayani Maswa, kata ya Binza, alishuhudia shule ya msingi yenye vyoo vinavyokosa maji, hali inayosababisha baadhi ya watoto kupangusia kinyesi kwenye kuta za vyoo baada ya kujisaidia.
Alisema hali hiyo ni tishio kubwa kwa usalama wa afya ya jamii.
“Miaka 64 ya uhuru, kilometa tano tu kutoka mjini, shule inakosa maji; jambo hili ni hatari sana. Kama serikali ya chama tawala inashindwa kupeleka maji hata chooni, itaweza nini kwa wananchi?” alihoji Mhe. Doyo mbele ya wananchi wa Kwimba.
Akiendelea kuzungumza, aliahidi kuwa iwapo wananchi watamchagua, serikali yake itahakikisha inalinda usalama wa afya za Watanzania na kizazi kijacho.Aidha, Doyo alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za NBS (2022), zaidi ya asilimia 30 ya vituo vya afya nchini vinakabiliwa na upungufu wa dawa muhimu, hasa vijijini.
Vilevile, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wagonjwa hulazimika kununua dawa kutoka sekta binafsi kutokana na uhaba wa dawa kwenye vituo vya umma.
Doyo aliongeza kuwa ripoti ya Benki ya Dunia (2022) inaonyesha uwiano wa daktari kwa wagonjwa nchini Tanzania ni 1:25,000, kiwango ambacho kiko chini sana ya viwango vinavyopendekezwa na WHO vya 1:1,000.
Alisema hali hiyo inawafanya Watanzania wengi kusubiri huduma ya kumuona daktari kwa muda mrefu, jambo linalosababisha athari kubwa za kiafya.
“Je, endapo kikizuka kipindupindu katika shule, watoto wetu hawatakuwa hatarini?” alihoji Doyo.
Akifafanua zaidi, Mhe. Doyo aliahidi kuwa serikali ya NLD itatekeleza sera mpya ya maji yenye malengo ya kuhakikisha kila kijiji na kata nchini vinakuwa na chanzo cha maji safi na salama ndani ya kilometa moja. Alibainisha kuwa shule na vituo vya afya vitapewa kipaumbele cha kupata huduma hiyo, huku serikali yake ikitumia teknolojia rafiki kama nishati ya jua kusukuma maji vijijini na kuimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji.
Aidha, Mhe. Doyo aliendelea kupinga mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima wa Kanda ya Ziwa, akidai ni mfumo wa unyonyaji unaowadhoofisha wakulima wadogo.
Kampeni za Chama cha NLD zimeingia rasmi mkoani Mwanza, katika muendelezo wa kumnadi mgombea wao wa urais, Mhe. Hassan Doyo.
No comments
Post a Comment