MHE. DOYO: AAHIDI KUTATUA CHANGAMOTO YA MAJI NA AFYA MKOANI MWANZA
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake mkoani Mwanza ambapo leo amefanya mikutano miwili ya hadhara katika Wilaya ya Misungwi, viwanja vya Soko la Zamani na Kata ya Usagaea.
Akihutubia maelfu ya wananchi, Mhe. Doyo alieleza changamoto kubwa zinazowakabili wakazi wa maeneo hayo, hususan matatizo ya huduma za afya na upatikanaji wa maji safi na salama.
Amesema licha ya kuwepo kwa hospitali wilayani humo, huduma zinazotolewa ni duni kutokana na ukosefu wa dawa, hali inayowafanya wananchi kuendelea kuteseka. Aidha, aliibua masikitiko yake kuhusu hali inayowakumba akinamama wajawazito wanaolazimika kwenda na ndoo za maji hospitalini wanapokwenda kujifungua kutokana na uhaba wa maji.
“Hili si jambo la utu. Mama mjamzito anapotakiwa kwenda na ndoo ya maji anapokwenda kujifungua, afya yake na ya mtoto wake huwekwa hatarini. Haiwezekani Misungwi izungukwe na ziwa, halafu maji ya kunywa na kutumia yakosekane. Hii haiingii akilini,” alisema Mhe. Doyo.
Mgombea huyo aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa Rais, atahakikisha wananchi wa Misungwi na maeneo mengine nchini wanapata huduma bora za maji safi na salama karibu na makazi yao, ili kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu kufuata maji.Aidha, Mhe. Doyo alisema zaidi ya asilimia 38 ya Watanzania bado hawana huduma ya uhakika ya maji safi ya bomba, akisisitiza kuwa tatizo hilo ni matokeo ya kutowajibika kwa Serikali iliyopo madarakani.
“Ni wakati wa kuiondoa CCM ili kukomesha tatizo la ukosefu wa maji. Wananchi wanastahili huduma bora na maisha yenye heshima,” alisema.
Kampeni za mgombea huyo zinaendelea, na kesho msafara wake unatarajiwa kufika mkoani Geita, kisha kuelekea Tabora na Kigoma.
No comments
Post a Comment