Mbeto : Sera za CCM msingi wa mageuzi ya maendeleo Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema sera zake zimejenga msingi wa uchumi imara Zanzibar na kubadilisha aina ya mfumo wa maisha kwa miaka minne iliopita .
Pia chama hicho kimeahidi kutekeleza tafsiri ya Siasa kutumikia Uchumi , Siasa safi na Uongozi bora, utakaokuza ustawi na maisha bora zaidi miaka mitano ijayo .
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo ,Khamis Mbeto Khamis , akiwa katika Kisiwa cha Tumbatu , Mkoa wa Kaskazini Unguja katika zoezi la uandikishaji wapiga kura.
Mbeto alisema Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi na serikali yake , amejipanga kimkakati ili kuacha alama ya uongozi na utumishi bora kwa Zanzibar na watu wake .
Alisema katika awamu ya kwanza minne iliopita , SMZ imejikita zaidi katika kusimamia mpango ya mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya maendeleo , kuinua huduma za kisekta na uwekaji bora wa mifumo ya kiutendaji Serikalini kwa viwango stahili .
" Wanasiasa hawa hawa wanaodhihaki utendaji wa smz majukwani na kudhani ni simulizi, wajiandae kuaibika. Watashuhudia mabadiliko ya kimaendeleo yatakayoacha alama kwa miaka mingi ijayo Unguja na P emba " Alisema Mbeto .
Kadhalika ,alisema wanaokosoa leo kwa jazba za kisiasa na kudai hakuna kilichofanyika , siku moja watakakuwa wa kwanza kusifu Zanzibar itakavyochupa kimaendeleo " Alisema Mbeto
Aidha alisema Rais Dk Mwinyi hatakatishwa tamaa kwa maneno ya udaku wa kisiasa , utapitapi wa vibaraka wenye uzezeta unaowafanya kupiga vita juhudi za maendeleo .
'Sera za CCM miaka mitano ijayo 2025 -2030 zitaibadili Zanzibar na kuipandisha chati kwa kiwango cha juu . Wanasiasa uchwara wataifumba midomo yao . Hapo ndipo kila mmoja atakapotafuta alipomfunga punda wake" Alisisitiza Mbeto.
Katibu huyo Mwenezi alikuwa ajibu baadhi ya maswali ya waandishi kwa anavyoutazama uongozi wa Rais Dkt Mwinyi miaka mitano ijayo ikiwa atashika tena madaraka .
"Kwanza nikuhakikishieni Rais Dk Mwinyi hatashindwa uchaguzi. Hata wapinzani wetu hilo wanalijua . Tunajivunia ufanisi wa kazi na utelelezaji wa sera zetu toka mwaka 2020 hadi oktoba Mwaka huu " Alisema Mbeto kwa kujiamini.
Mwenezi huyo pia amezisifu Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya za Kaskazini ' A' na 'B" Mkoa ya Kaskazini Unguja kwa kusimamia usalama na kuhakikisha kila aliyekidhi vigezo vya sheria amepata nafasi ya kujiandikisha.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni