Zinazobamba

𝗞𝗜𝗡𝗢𝗡𝗗𝗢𝗡𝗜 𝗬𝗔𝗪𝗔𝗡𝗢𝗔 𝗩𝗜𝗢𝗡𝗚𝗢𝗭𝗜 𝟭𝟮𝟬𝟬+ 𝗪𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗔 𝗡𝗔 𝗠𝗔𝗧𝗔𝗪𝗜 𝗞𝗨𝗘𝗟𝗘𝗞𝗘𝗔 𝗨𝗖𝗛𝗔𝗚𝗨𝗭𝗜 𝗠𝗞𝗨𝗨 𝟮𝟬𝟮𝟱


UVCCM Wilaya ya Kinondoni imeendesha semina maalum ya mafunzo ya uongozi kwa zaidi ya viongozi 1,200 wa Kata na Matawi kama sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Mafunzo haya, yaliyofanyika tarehe 23 Februari 2025, yalifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Ndugu Shaweji Mkumbula, ambaye aliwasihi vijana kuepuka makundi ya wanasiasa wasio na nia njema na badala yake wajikite katika kujenga chama na jumuiya yao kwa umoja na mshikamano.

“Vijana mnapaswa kuelekeza nguvu zenu katika kuimarisha CCM na UVCCM, siyo kushiriki katika makundi yanayopotosha au kugawa umoja wetu. Chama chetu kinategemea nguvu zenu, mshikamano na uvumilivu wenu kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo mwaka 2025,” alisema.

Katika hotuba ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya, Ndugu Abdulrahman Kassim, aliwataka viongozi vijana kutumia maarifa waliyopewa kwa vitendo ili kujenga UVCCM imara na chenye ushawishi mkubwa. "Vijana wa CCM hatupaswi kuwa mashabiki wa siasa tu, bali tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha, kushiriki kwa kugombea na kukisaidia chama chetu kushinda kwa kishindo. Mafunzo haya yatakuwa na maana endapo tutayatumia kujijenga na kuimarisha chama chetu na Jumuiya yetu," alisema.

Aidha, aliwahimiza viongozi hao kuwa mfano wa nidhamu na utendaji mzuri akisisitiza kuwa, "Ushindi wa CCM mwaka 2025 hautatokea kwa bahati tu, bali unahitaji juhudi, mshikamano na utayari wetu kama vijana wa UVCCM. Ni lazima tuhakikishe kuwa kila kijana anakuwa sehemu ya harakati hizi kwa kuhamasisha uandikishaji na uboreshaji wa taarifa kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura litakaloanza Machi 17, 2025, hadi Machi 23, 2025, kwa mkoa wa Dar es Salaam."Awali, Katibu wa UVCCM Wilaya, Ndugu Amosi S. Richard, alisema semina hiyo ni utekelezaji wa Katiba ya CCM, Kanuni za UVCCM na maadhimio ya Baraza la UVCCM Wilaya ya Kinondoni, yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi za chini ili kuongeza ushawishi wa chama kwa vijana kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

UVCCM Kinondoni itaendelea kuwaandaa viongozi imara, wabunifu na wenye uwezo wa kuhimili changamoto za kisiasa kwa maslahi mapana ya vijana na taifa.#UVCCMKinondoni #TunaendeleaNaMama

Hakuna maoni