Zinazobamba

WANANCHI MTAA WA MZINGA WAOMBA KUONDOLEWA KIFUSI KINACHODHANIWA KUWA NA KEMIKALI YENYE ATHARI

                Dc wa Ilala Edward Mpogolo

Na Mussa Augustine 

Wakati Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mzinga, Kata ya Mzinga wilayani Ilala, Daniel Nyaiko, akibainisha kwamba Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo,tayari amepeleka wataalamu kupima udongo unaolalamikiwa na wananchi wakidhani unaweza kuwa na kemikali inayoathiri makazi yao, Mkuu huyo wa Wilaya amekanusha taarifa hiyo.

"Wewe ndio unanipa taarifa hizi, mimi sijui, kwangu hazijafika, inawezekana hiki ni kipindi cha uchaguzi, pengine wananchi hao hawamtaki Mwenyekiti, sasa waambie wakajiandikishe ili waweze kupiga kura,ili waweze kubadilisha uongozi" amejibu DC Mpogolo wakati akizungumza na Mwandishi wa habari.

Nakuongeza kuwa "Kwa sababu ulitakiwa kuwauliza hicho kifusi, kimetoka wapi au katika kiwanda gani hapo ndipo tuanze uchunguzi".

Wakati Mpogolo akisema hana taarifa hiyo, awali mwenyekiti wa mtaa huo, Nyaiko  alimweleza mwandishi wa habari  hizi kwamba kufuatia wasiwasi uliotanda kwa wananchi kuhusu kifusi kilichomwagwa barabani wakidai kuwa na kemikali kutokana na athari zinazojitokeza, tayari jopo la wataalamu nane kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo walifika jana, Septemba 24, 2024 na wamechukua sampuli ya udogo unaolalamikiwa kwa ajili ya kupima  na Ijumaa Septemba 27, 2024 majibu yatarejeshwa kwa  wananchi.Malalamiko ya wananchi kuhusu kifusi hicho ambacho kimemwagwa katika barabara ya Nyangasa eneo la Kwanyoso yalianza tangu, 2021 baada ya athari ya bati za nyumba zao kuanza kupata kutu na kutoboka kabla ya muda sahihi.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Matokeo Charles, amesema "baada ya kifusi hicho kumwagwa, mvua ziliponyesha tu maji yaliyotiririka kutoka kwenye bati yalionesha kuwa na chembeche zenye mn'gao.

"Hali hiyo ikafuatiwa na mabati kupata kutu na kutoboka kabla ya wakati kwa kuwa zilikuwa mpya na zisingeweza kupata kutu kwa haraka na kutoboka, pia wakati kifusi hicho kinamwagwa kilikuwa na vipande vingi vya chuma ambavyo viliokotwa kama chakavu na kuuzwa" ameongeza.

Pia alisema kwamba baada ya kadhia hiyo kujitokeza walifiksha taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa huo, ambaye inadaiwa ndiye aliyekimwaga eneo hilo kwa ajili ya kufukia mashimo yaliyokuwa kwenye barabara hiyo.

Ameongeza licha ya kufikisha malalamiko hayo wakadai hayakufanyiwa kaz,  badala yake waliambiwa kuwa ni wapinzani wa kisiasa na wapinga Maendeleo.

Kutokana na kutosikilizwa waliamua kuyafikisha malalamiko yao kwa njia ya barua kwa diwani wao, Mtendaji Kata, Mkurugenzi wa Jiji la Ilala, Kwa Mkuu wa wilaya hiyo wa wakati huo,  Mwilabuzi Ludigija, pamoja na  Baraza la Taifa la Mazingira( NEMC).

Matokeo, anadai baada ya hatua hizo, NEMC walipeleka  wataalamu wao na kuchukua sampuli ya mchanga na hadi sasa hakuna majibu yaliyorejeshwa kwao ili hali athari zinazidi kuongezeka" amesema.

 Pia anafafanua kwamba wakati changamoto hiyo inajitokeza kulikuwa na nyumba zipatazo 19 ambazo ziliathirikia na anadai zinakaribia 40 ambazo mabati yametoboka nakusababisha hasara kubwa kwa wananchi hao.

Naye Mjumbe wa Kamati katika Msikiti wa Nurhuda ambao upo pembezoni mwa barabara hiyo, Ustadhi Juma Ally ,amesema baada ya adha hiyo kutokea, tayari wamebadilisha bati ingawa nazo kwa muda mfupi zimeanza kupata kutu na kutoboka.

"Tunaomba, Rais atusaidie,watendaji wake huku chini wanaonekana wameshindwa kutusaidia,sisi ni wananchi wake, hatuna pesa kubadilisha bati kila mara,tumetoa malalamiko yetu kwa muda mrefu lakani hatusaidii na hawa wasaidizi wake  "amesema.

Pia, Ombi Sanga mkazi wa mtaa huo, amesema kuwa inashangaza wanapotoa malalamiko yao kwa viongozi wao wanasemwa kwamba wao ni wapinga maendeleo na kwamba wanatumiwa kisiasa jambo ambalo amedai sio la kweli, wanachotaka wao ni kifusi hicho kiondokewe na kiwekwe kingine.

"Sijui nini kinawashinda wakati athari zinazidi, tunamuomba Rais Dkt Samia atusikilize ili atusaidie kutuondolea athari hii kwani wasaidizi wake wameshindwa, amesema.

"Kwakweli hali hii inatuumiza mno kwa muda mrefu sasa, tunaomba Mama( Rais Samia) atusaidie, kwa maana viongozi wa huku chini wameshindwa kabisa kutusaidia,tunateseka na changamoto hii" amesema.



Hakuna maoni