Zinazobamba

TASAC,NBS ZAZINDUA RIPOTI YA KWANZA YA SENSA YA VYOMBO VIDOGO VYA USAFIRI MAJINI

 


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Atupele Mwakibete akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Sensa ya Vyombo Vidogo vya Usafiri Majini katika eneo la Tanzania Bara, 2021. 

 NA Mussa Augustine. 

Shirika la  Uwakala wa Meli nchini (TASAC) kwa kushirikiana  na ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) limezindua ripoti ya sensa ya vyombo vidogo vya usafiri Majini ambayo ni ya kwanza kuwahi kufanyika Nchini Tanzania,pamoja na  Nchi za Afrika Mashariki na kanda wa Nchi za Kusini mwa Africa (SADC ).

Akizungumza Wakati wa  uzinduzi wa ripoti hiyo Julai 11,2023  Jijini Dar es salaam Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi anayesimamia Sekta ya Uchukuzi Atupele Mwakibete amebainisha kuwa  ripoti hiyo itasaidia kuboresha sera,kubainisha fursa zilizopo katika kukuza uchumi wa Taifa na watu wake kupitia uchumi wa bluu.

 Aidha Naibu Waziri Mwakibete amewataka wadau mbalimbali kutumia taarifa  hiyo kibiashara kwa kuangazia maeneo yenye vyombo vingi vya usafiri wa majini ili kufungua biashara za uuzaji wa vipuri vya boti,maboya,injini na vifaa vingine.


"kwa mujibu wa taarifa ya sensa jumla ya idadi ya vyombo vidogo vya majini ni 52,189, pia kuna jumla ya mialo 885,idadi ya vyombo vidogo vya majini vyenye urefu wa mita nne au zaidi kwenye maeneo ya maji ni 45,976,kati ya hivyo Asilimia 53.65% vipo Ziwa Victoria, 13.41% vipo Bahari ya Hindi,10.28% vipo Ziwa Tanganyika,7.65 vipo Ziwa Nyasa na Asilimia 15.1% vipo katika maeneo mengine ya maziwa na mabwawa nchini" Amesema Mwakibete .


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)     Kaimu Mkeyenge amesema wakati wa  uandaaji wa sensa hiyo wameshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),Wizara ya ujenzi na uchukuzi,TAMISEMI , Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya Uchukuzi.

“Baada ya kukamilika kwa sensa hii,tumeweza kuunda kanzi data maalumu inayorahisisha kuvitambua vyombo hivyo,wamiliki na maeneo vilipo na kurahisisha utambuzi wa vyombo na hali yake na endapo kikitapata majanga kuweza kukifikia kwa haraka na kutambua ni chombo kipi kimehusika kwenye ajali au changamoto yoyote majini”Amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa TASAC Kaim Mkeyenge

Hata hivyo  Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema ni mara ya kwanza NBS imeshiriki katika sensa ya vyombo vya majini hivyo wameipongeza TASAC kwa hatua hiyo na kuongeza kuwa kanzi data iliyoundwa itasaidia sana Wafanyabiashara,wadadisi na watafiti mbalimbali kufanyakazi yao kwa urahisi zaidi.


Hakuna maoni