Zinazobamba

TAWA, GREENCOP DEVELOPMENT PTE Ltd ZASAINI MAKUBALIANO YA BIASHARA YA HEWA UKAA (CO2).

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka  ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesaini makubaliano ya awali (MoU) ya kufanya Biashara ya Hewa Ukaa (Carbon dioxide -CO2). na Kampuni ya Kigeni ya GreenCop Development PTE LTD  leo Mei 18, 2023 jijini Dar es Salaam.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA. Mabula Misungwi Nyanda na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya GreenCop Development PTE Ltd Bw. Jean-Jacques Coppee na kushuhudiwa na , Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abassi, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamisi Semfuko, Mjumbe wa Bodi ya TAWA, Profesa  Suzana Augustino

Zoezi hilo pia limeshuhudiwa  na Mwanasheria Mwandamizi wa TAWA, Stephen Mwamashenjele, Manaibu Kamishna,  Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa TAWA na Maafisa wa juu wa Kampuni hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi ameipongeza TAWA kwa kusimamia na kusukuma mchakato huo uliopelekea kutiwa saini.

“Wizara inawahakikishia TAWA na Wabia wetu kutoka kwenye hatua hii ya MoU kwenda kwenye mkataba kamili kama kutakuwa na vikwazo au mkwamo wa aina yoyote Wizara iko tayari kuyatatua.” Alisema Dkt. Abbasi.

Awali Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA  Mabula Misungwi Nyanda alisema kuna makampuni mengi yameleta maombi ya kuwekeza kwenye eneo hili, na matatu yako kwenye hatua za mwisho

“Kampuni ya GreenCop PET Ltd inahusisha maeneo matatu ambayo ni pori la Akiba la Selous, Kilombero na Msanjesi na haya ndiyo tutaanza kufanya nayo kazi.” Amefafanua na kuongeza..“Kilichofanyika leo ni makubaliano ya awali ambayo yanafungua milango ya kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa nyaraka za mradi na hapo ndipo itafuata hatua ya kusaini mkataba utakaowezesha kuanza biashara yenyewe.” 

Kamishna Mabula amewahakikishia watanzania kuwa uwekezaji huo hauna athari za kimazingira kwenye mapori yanayosimamiwa na TAWA  zaidi ni kuzalisha faida.

Amesema katika makubaliano hayo ya awali imeanishwa muda kuwa ni kati ya mwaka mmoja hadi miwili.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Hamisi Semfuko amesema makubaliano hayo ni muhimu katika historia ya TAWA na Serikali kwa ujumla. 

“Tunaamini biashara ya "Carbon" ni mradi mpya katika thamani ya kiuchumi na uhifadhi na itanufaisha pia wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi.” Amesema. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya GreenCop Development PTE Ltd Jean-Jacques Coppee ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia makubaliano hayo kusainiwa.

“Makubaliano haya ni muunganiko wa maono yatakayopelekea pato la kiuchumi la muda mrefu katika mapori ya Selous, Msanjesi na Kilombero kwa kulinda uoto wa asili na kupambana na mabadiliko ya tabia Nchi.

“”Lakini wakati huo huo mradi utaleta faida za kiuchumi kwa kwa jamii inayozunguka maeneo ya hifadhi kwa kuuza "carbon credits.” amesema

 

Hakuna maoni