NA MWANDISHI WETU

KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amewakabidhi vyeti wahitimu zaidi ya 200 wa mafinzo ya Pilisi Jamii Kata ya Kawe Mkoa wa Kipolisi Kinondo.

Akizungumza baada ya kukabidhi vyeti hivyo SACP Muliro amesema kwamba kazi ya masuala ya kiusalama zinahitaji maarifa ya kiutaalamu ikiwemo kufahamu sheria.

Hivyo amesema kwamba wahitimu hao watakuwa msaada muhimu katika kuongeza nguvu za kuimarisha usalama kwani Jeshi la Polisi peke yake haliweze kuhakikisha usalama wa kila mahali hapa nchini.

“Mfano Mkoa wa Dar es Salaam linawatu zaidi ya milioni 5, hivyo lazima tuboreshe mifumo ya kiusalama. Nimpongeze sana Mtume Mwanposa kwa kuwa sehemu ya kushirikiana na Polisi kwa kuona umuhimu wa kuwepo vikundi vya polisi jamii kwa ajili ya kushirikiana na Jeshi la Polisi,” amesema SACP Muliro.

Amesema Polisi Jamii hao wamewapa mafunzo ya kuelewa falsafa ya Polisi Jamii, kujua kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia kwani wanaweza kusaidia katika kudhibiti vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.

“Tunaamini makundi haya yaliyoandaliwa yatakuwa mabalozi wazuri wa falsafa ya Polisi Jamii, mmefundishwa msijiingize katika matumizi ya nguvu katika kutekeleza majukumu yenu,” ameongeza SACP Muliro.

Hivyo amewataka kushirikiana na Jeshi la Polisi katika ulinzi wa usalama na kuahidi kwamba Jeshi la Polisi litawapa ushirikiano.

Kwa upande wake Kiongozi wa Huduma ya Inuka Uangaze(Rise and Shine) Mtume Boniphace Mwamposa amesema kwamba Polisi Jamii hao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi watafanya kazi nzuri ya kulinda usalama.