Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ACT Wazalendo Abdul Nondo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

NGOME ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo imasema haijaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na ubadhilifu wa fedha za umma uliobainishwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Aprili 9 mwaka huu Rais Dkt. Samia alivunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TET), alitengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na kuagiza Watendaji wa Taasisi kupitia na kujibu hoja za CAG katika maeneo yao na watakaobainika wachukuliwe hatua.

Akuzungumza na waandishi wa habaro leo Aprili 12, 2023 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa Abdul Nondo amesema hawajaridhishwa na hatua hizo, hivyo ametaka hatua zaidi zichukuliwe ili kukomesha vitendo hivyo vya ubadhilifu wa fedha za umma.

“Hutajaridhishwa na hatua hizi za ujumla alizochukua Mh. Rais Samia kwani mara zote watendaji wa Serikali wana tabia na mtindo wa kulindana na mara zote hawatilii maanani magizo ya namna hii yanayotolewa na viongozi,” amesema Nondo.

Hivyo Nondo ameeleza kwamba Ngome ya Vijana imetoa wito kwa Serikali na Bunge kuchukua hatua muhimu ambazo ni kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Nyingine ni Rais aunde Tume Huru ya Kijaji kwa ajili ya uchunguzi wa matumizi mabaya ya Ofisi na Maadili ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Buswalo Mganga na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ajiuzulu au awajibishwe na mamlaka ya uteuzi.

Nondo ameeleza hatua nyingine za kuchukulowa kuwa ni Bunge liunde Kamati teule kwa ajili ya kuchunguza ubadhilifu mkubwa katika Shirika la Reli Tanzania (TRC) kupitia manunuzi ya kwenye Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati (SGR) ili kuchunguza sababu za TRC kutoa tenda bila ushindani jambo ambalo limepelekea gharama za ujenzi kuongezeka maradufu.

Ameongeza hatua nyingine ni Taasisi zilizowekwa awali chini ya Ofisi ya Rais ziondolewe ili kuweka uwajibikaji na ziwe zinakaguliwa na CAG.

Ametaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na TAKUKURU kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya 2007 kifungu cha 47 (1 na 2) kinaeleza kuhusu TAKUKURU kufanyiwa ukaguzi kwani inatengewa fedha na Bunge, lakini haijawahi kukaguliwa.

Hivyo amesema ni matarajiao yao kuwa madai hayo na mengine ya hatua muhimu za kiuwajibikaji yatafanyiwa kazi mara moja.

Hata hivyo Nondo amedai kwamba  hadi kufukia Aprili 18, 2023 kama hatua zaidi zitakuwa hazijachukuliwa watatoa tamko la maandamano ya amani nchi nzima kupinga wabadhilifu wa fedha za umma kuendelea kuwepo maofisini.