Zinazobamba

 

Na Mussa Augustine.

Chama cha Alliance for Demecratic Change (ADC) kimeitaka Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha zinadhibiti mfumuko wa bei ambao umewafanya Wananchi kuishi katika mazingira magumu.

 Kauli hiyo imetolewa leo Novemba 22, 2022 na Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Hamad Rashid akifungua Mkutano wa Bodi ya Uongozi wa Chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 Rashid amesema kwamba kila siku kumekuwepo na kupata kwa mfumuko wa bei licha ya juhudi kubwa inayofanywa na Serikali ya kuudhibiti ikiwemo kutoa ruzuku kwa bidhaa mbalimbali ikiwemo mafuta.

 “Tunaiomba BoT ihakikishe bei ya Chakula inarudi pale ilipokuwa awali ya shilingi kati ya 1900 na shilingi 2000 kwani kwa kupanda huku kunatufanya kurudi kwenye umasikini. Kama wakishindwa waje kwetu tutawapa ushauri,” amesema Rashid.

Kiongozi huyo wa ADC pia amezungumzia hali ya Demokrasia nchini,ambapo amewashukuru na kuwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Hussein Mwinyi kwa kushirikiana na wadau wa siasa na kuunda vikosi kazi kwa ajili ya kuona namna ya kuboresha ufanyaji wa siasa nchini.

 Hata hivyo ameomba Serikali kuhakikisha inaruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa kwani mikutano ya hadhara ndiyo uhai wa vyama vya siasa vyenye malengo ya kushika dola.

 “Tunaomba mikugano ya hadhara iruhusiwe mapema iwezekanavyo, uhai wa vyama vya siasa ni mikutano ya hadhara, kama kuna mahali kwenye sheria kunatakiwa kurekebishwa basi palekebishwe ili mikutano iruhusiwe,” ameongeza Rashid.

 Akizungumzia kuhusu Sekta ya Afya Hamad Rashid ameishauri Serikali kuingia mikataba na watengenezaji wa vifaa tiba ili iwahakikishie upatikanaji wa vifaa tiba hivyo katika hospitali za nchini.

 Kuhusu chakula amewataka Watanzania kuhakikisha wanazalisha chakula cha kutosha na kuhakikisha kila pahala panakuwa na matunda.

 Akizungumzia uhaba wa maji nchini Kiongozi huyo wa ADC ameitaka Serikali kuhakikisha inawekeza katika uvunaji wa maji, lakini pia kuwa na mitambo ya kusafishia maji ili yapatikane kwa wingi.

 Hata hivyo amebainisha kuwa chama hicho kipo tayari kushirikiana na serikali katika kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo mfumuko wa bei ambao unawafanya watanzania kuwa masikini.

Hakuna maoni