Zinazobamba

DC malinyi atoa maelekezo somo la EDK katika shule za umma



Afisa Tarafa wa Malinyi Ms Rehema Rajabu akizungumza na walimu wa somo la elimu ya dini ya Kiislam (EDK) Wilayani humo. Walimu zaidi ya 200 walihudhuria mkutano huo uliolenga kuwajengea uwezo katika kulifundisha kwa weledi.

Sehemu ya Walimu na waumini wa Kiislamu wakimsikiliza   Afisa Tarafa ya Malinyi Ms Rehema Rajabu. 

Meneja wa Islamic Education Panel Abdulswaburi akifafanua jambo kwa wanasemina.  Mtaalam huyo amesema somo la EDK ni zuri kwenye kujenga maadili ya Viana. Mkazo unatakiwa kuwekwa katika shule za umma. 





Na Mwandishi wetu

Mkuu wa wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro ametoa rai kwa walimu wa umma wenye uwezo wa kufundisha somo la elimu ya dini ya Kiislam (EDK) kufanya hivyo mara moja huku akisisitiza kuwa hakuna haja ya kuona haya, woga au hofu yeyote.

Akizungumza katika semina ya walimu wa somo hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Afisa Tarafa ya Malinyi Ms Rehema Rajabu amesema haoni sababu ya walimu kuwa na hofu ya kufundisha elimu ya dini huku wakijua wazi kuwa kufanya hivyo sio kosa kisheria

 

“Nitashangaa sana kama bado wapo walimu wenye uwezo wa kufundisha somo hili lakini wanajificha kwa kuogopa watu, serikali inapenda kuona jamii inalelewa katika maadili mema na somo hili linajikita kwenye maadili, kwa nini sasa mwalim uogope kutoa elimu yako,” alihoji Ms Rehema

Aidha, Rehema amewahamasisha wananchi wa Wilaya ya Malinyi kufanyia pupa mambo ya heri ili kukabiliana na tatizo la maadili ambalo linaoota mizizi kila kukicha.

“Hapa wilayani bado mwamko wa dini uko chini, wengi wamejikita kwenye utamaduni wa asili, nadhani muda umefika wa kubadirika, tuanze kuwapeleka vijana wetu madras kujifunza wajibu wao na sababu za kuletwa duniani, naamini nyoyo za watoto wetu zitajengeka kimaadili kwani watakuwa ni watoto wenye hofu na Mungu,” aliongeza.

Vilevile, ameitaka jamii ya Malinyi kuwa na moyo wa kutoa mali zao kwa ajili ya kuendeleza dini, na kwa kuanzia ameshauri kutatua changamoto ya vitabu vya EDK ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi

“Walimu wamesema hapa tunalo tatizo la vitabu vya EDK, kwa kuanzia vinatakiwa vitabu vyenye thamani ya Mioni tatu, jambo hili lipo ndani ya uwezo wetu, tutowe mali zetu ili vijana wetu wapate elimu hii muhimu,” alisema

Kuhusu jambo ambalo linamuhudhunisha, Ms Rehema amesema licha ya ukweli kuwa jamii ya Malinyi ni tajiri lakini wamekuwa na moyo mgumu wa kujitoa kwenye mambo ya dini.

Alisema kitendo hicho kimepelekea mwamko wa dini kuwa chini na hivyo vijana wengi wa eneo hilo wamejikuta wakiitanguliza Zaidi dunia kuliko akhera yao.

Katika hatua nyingine walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo wameungana na Kaimu Mkuu wa Wialaya huyo, Ms Rehema kwa kusema kuwa bado kuna changamoto ya somo la dini wilyani hapo.

Mmoja wa walimu hao, Bw. Fadhiri Chuma, Mwalimu wa shule ya sekondari Mtimbira alifichua kuwa kunahitajika vitabu vya kutosha ili kufundisha somo hilo, kwani walimu wapo wa kutosha shida ni vitendea kazi.

Alisema licha ya uwepo wa vipindi vya dini, lakini wamejikuta wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa kukosa miongozo ya somo la EDK hali inayopelekea somo hilo kuwa geni kwa watoto wa Malinyi

Pia Mwalim Shaabani Mandanda kutoka shule ya msingi Nawigo iliyopo Wilaya ya Malinyi amewaomba waislam na jamii kwa ujumla kujitoa kwa hali na mali ili vitabu vya elimu ya dini vipatikane na vijana waanze kupatiwa mafunzo yatakayo wasaidia katika maisha yao.

 

Hali ya somo la EDK Malinyi…

Aidha, akizungumzia hali ya somo la EDK Malinyi mmoja wa wazazi wa eneo hilo, Matano Matano alisema ni mbaya sana kwani Wilaya nzima haina watoto wanaosoma somo hilo

“Mtoto akichukua somo hilo kwake inakuwa ni mtihani mkubwa, hakuna Mwalimu wa kufundisha, mwanangu amejitahidi kulichukua kwa sababu msingi wake umejengwa kwenye dini akiwa Zanzibar lakini walimu wa kufundisha ni mtihani mkubwa,

Nimejaribu kuwafuata walimu kadhaa ambao najua wanafahamu kidogo kuhusu EDK kwa kuahidi kuwalipa kwa mwezi 100,000, ajabu ni kwamba hakuna aliyekuwa tayari

Kila mmoja anatoa udhuru, yaani 100,000 kwa mwezi, alafu unafundisha kwa wiki mara moja, watu wanaona shida, vipi mtoto anaweza kupenda somo hilo,” alisema kwa uchungu Matano

Kwa upande wake Amiri wa Islamic Education Panel Kanda ya Mashariki, Abuswaburi akielezea maendeleo ya somo hilo amesema maendeleo ni ya kuridhisha ukilinganisha na miaka ya nyuma.

 

Amesema kwa mujibu wa Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Dini ya Kiislamu nchini (EDK) kwa mwaka 2022 kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka wastani wa asilimia 49.78 kwa mwaka 2021 hadi kufikia wastani wa 66.77.

 

Aidha idadi ya watahiniwa nayo imeongezeka kutoka  watahiniwa 126,088 mwaka 2021 hadi kufikia watahiniwa 142,522 mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 16,434 sawa na asilimia 13.3

 

Aidha Wanafunzi 3,567 wamefanya vizuri katika mitihani yao kwa kupata Daraja A huku waliopata Daraja B wakiwa 22,587 na C wakiwa 69,012.

 

Akifafanua ufaulu huo alisema kwa ujumla waliofaulu kwa kupata Daraja A hadi C ni watoto 95,166 sawa na asilimia 66.77, huku watoto 47,356 sawa na asilimia 33.23 wakipata Daraja D na E. Daraja D watoto 45,781 na E watoto 1,575.

 

Naye Mratibu wa Islamic Education Panel Taifa (IEP), Suleiman Daudi, amewakumbusha waislam wa Malinyi na Taifa kwa ujumla kutoa mali zao kwa ajili ya kutengeneza nyoyo za kizazi cha kesho kimaadili.

Hakuna maoni