Zinazobamba

Waziri Mwakibete amewataka wananchi wanaofanya shughuli za kiuchumi kando mwa njia ya reli waondoke

Na Mussa Augustine.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amewataka wananchi wanaofanya shughuli za kiuchumi na Kijamii kando mwa njia ya reli waondoke kuupisha mradi wa treni ya mwendokasi itumiayo umeme(SGR).
Waziri Mwakibete ametoa amri hiyo leo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Usalama wa reli yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, yenye kaulimbiu "Chukua tahadhari ,treni zina mwendo wa haraka,ni hatari "

Amesema wananchi wanatakiwa watambue uwepo wao kukaa maeneo hayo ni hatari kwani treni hizo zina mwendo kasi na kuepusha ajali ambazo zitaweza kuzuilika.

Aidha ameongeza kuwa shughuli hizo zinazofanyika maeneo hayo pembezoni mwa njia zinaharibu miundombinu kwani serikali tayari imeshatumia takribani trilion 7 katika mradi wa SGR.

Pia amewataka watumishi waliopo kwenye taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ikiwemo TRC, TAZARA, LATRA na TANROADS kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo na kuwataka wawe waaminifu na kuondoa uzembe wawapo kazini kwani uzembe wao unachangia kusababisha ajali na kugharimu maisha ya wananchi.

Waziri Mwakibete ameliagiza Shirika la reli TRC kuhahikisha linashughulikia changamoto zinazowakabili wafanyakazi wake ikiwemo malimbikizo ya mishahara ili kuwezesha wafanyakazi waweze kuwa na ari ya kujituma kufanya kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini( LATRA) Mhandisi Habibu Suluo amesema kuwa mamlaka hiyo itahakikisha inasimamia nakulinda usalama wa wananchi katika usafiri wa reli.

Mhandisi Suluo amewataka wananchi kila mmoja awe mlinzi kwa mwenzake katika uhujumu wa miundombinu ya reli ,kwani reli ni maendeleo katika kulijenga Taifa.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa shirika la reli Tanzani (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwekeza katika sekta ya reli nchini kwa ujenzi wa reli ya kisasa SGR ,kwani kupitia mradi huo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika shughuli za kiuchumi na mifumo ya ishara na mawasiliano.

Mhandisi Kadogosa  katika kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa reli tayari wameanza kutoa elimu nakwamba wataweka uzio katika njia nzima ipitayo reli ili kulinda usalama wa watu na wanyama. 

Hakuna maoni