Ni msimu wa ukame, wananchi wapewa angalizo TMA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania TMA, Dkt Agnes Kijazi amewashauri wadau wa mamlaka hiyo kujipanga vizuri kukabiliana na msimu wa mvua hafifu unaotarajiwa kuwepo katika kipindi cha msimu wa vuli unaoanza Oktoba hadi Disemba 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari Makao
Makuu ya Mamlaka hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam, Dkt Kijazi alisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa
katika msimu wa vuli wa mwaka huu kutakuwa na kipindi kirefiu cha ukavu.
Alisema kutakuwa na mvua za chini ya wastani
hadi wastani na kusababisha ukame kwa baadhi ya maeneo na kuwashauri wakulima
na wafugaji kujipanga kwa kupanda mazao yanayostamili ukame lakini pia kuweka
malisho ya ziada ili kuepuka migogoro.
“Kwa
ujumla mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi
ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Msimu unatarajiwa kuanza
kwa kuchelewa na kuambatana na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
Vipindi virefu zaidi vya ukavu vinatarajiwa
katika miezi ya Oktoba na Novemba 2022, hata hivyo vipindi vya ongezeko kidogo
la mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache hususan wiki ya tatu na
ya nne ya mwezi Disemba, 2022.
Kwa kawaida msimu wa mvua za Vuli huisha mwezi
Disemba, hata hivyo, kunatarajiwa kuwepo na mwendelezo wa mvua kwa mwezi
Januari, 2023,” alifafanua Dkt Kijazi.
Aidha
alisema kwa Kanda ya Ziwa Viktoria hasa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza,
Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za
Kibondo na Kakonko) kutakuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kwamba
mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2022. Aidha,
katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Simiyu mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki
ya nne ya mwezi Oktoba, 2022. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2023.
Kwenye ukanda wa Pwani ya Kaskazini hasa mikoa ya Morogoro, Pwani, visiwa vya
Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba nako
zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na mvua zake zitaanza
kunyesha kati ya wiki ya nne ya mwezi
Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022 na kuisha kwake Januari 2023.
Pia nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Mikoa
ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kutakuwa na mvua za chini ya wastani hadi
wastani na zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya
kwanza ya mwezi Novemba, 2022.
Katika hatua Mtaalam huyo wa masuala ya hali
ya hewa ameishauri jamii kutumia chakula kwa uangalifu, toka ngazi ya kaya hadi
taifa kwani msimu ujao ni wa ukame.
Aidha wadau wa Sekta ya mifugo, wavuvi,
alisema sekta hiyo itakabiliwa na uhaba wa upatikanaji wa maji hivyo migogoro
na watumiaji wengine wa ardhi inaweza kujitokeza, kwa hiyo amewataka wafugaji kujitahidi
kuhifadhi malisho pamoja na kufuatilia maelekezo yanayotolewa na maafisa ugani
na kujenga tabia ya kufuatilia utabiri wa mamlaka kujua hali inavyokwenda
Pia kwenye Sekta ya utalii na wanyama pori,
Dkt Kijazi alisema wanyama pori wanaweza kutoka porini kutafuta malisho sehehmu
zingine kwa sababu ya kukosa malisho hifadhini na kuzishauri mamlaka kutoa
elimu ili kuwakinga watu wanaozunguka maeneno yao na hatari ya kuvamiwa na
wanyama
Kwenye upande wa Usafiri na usafirishaji,
alisema ni muda mzuri wa kuendeleza mipango ya uboreshaji wa miundo mbinu,
ujenzi unaoendelea basi ufanyike kwa kufuata utabiri wa hali ya hewa.
Nao waandishi wa habari wametakiwa kuendelea
kuhabarisha umma habari sahihi kutoka mamlaka kwani kufanya hivyo kunaongeza
elimu kwa umma.
“Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia,
kupata na kusambaza taarifa sahihi za mwenendo wa msimu wa Vuli pamoja na
taarifa zilizohuishwa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA),” alisema
Pia amewashauri wanahabari kutafuta na
kutumia ushauri wa kisekta kutoka kwa wataalam wa sekta mbalimbali ili kuandaa
na kusambaza makala za taarifa za kisekta kwa lugha nyepesi inayoeleweka na
isiyoleta taharuki, kwa lengo la kuijulisha na kuielimisha jamii juu ya
matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika kujikinga na madhara
yanayoweza kujitokeza.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni