Zinazobamba

Ukweli kuhusu kitabu cha sheikh Ponda huu hapa, achambua Mbivu, mbichi

 




Na Suleiman Magali

Ikiwa imebaki siku mbili kitabu cha Juhudi na Changamoto kilichoandikwa na Sheikh Ponda Issa Ponda kuzinduliwa, Mwenyekiti ambaye anaratibu kongamano la uzinduzi wa kitabu hicho amefichua kuwa kitabu hicho  kimejaa ukweli na uhakika huku rejea na data zilizotumika zikiwa za kuaminika.

Pia alisema, kitabu hicho kinachosubiriwa kwa hamu na watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kimepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau licha ya kwamba bado hakijazinduliwa.

Akizungumza na gazeti imaani, Mwenyekiti huyo, Bw. Ibrahim Zuberi Mkondo alisema kitabu kimepata mwitikio mkubwa baada ya watu kupiga simu kwa wingi wakikiulizia licha ya kwamba bado hakizazinduliwa.

Aidha kuhusu maandalizi tayari yameshakamilika na zoezi lililobaki ni kuzinduliwa siku ya Jumapili, katika ukumbi wa Peacok Hotel, Dar es Salaam.

Pia akizungumzia kuhusu kitabu hicho, Mkondo alisema Kitabu kimeeleza mambo mengi na mazuri, kimeeleza juhudi za waislam kabla na baada ya uhuru na changamoto ambazo waislam wamekuwa wakipitia katika kila hatua.

“Tunapoeleza juhudi na changamoto maana yake waislam na wasio waislam watasoma walichokifanya viongozi/masheikh toka enzi hizo, watapitishwa kwenye mipango na mikakati ambayo imekuwa ikifanyika katika kuleta mabadiriko kwenye jamii ya kiislam,” alisema

Tunapoeleza changamoto watu wafahamu, kuwa tumejadiri kwa kina changamoto ambazo waislam wamepitia katika kila zama, lengo ni kuwafanya watu wasirudi nyuma.

Tunataka kuona wanapojaribu kuliendea jambo wafahamu kuwa linaweza kuwa na changamoto zake na wanapaswa kujiandaa nazo ili kuzishinda na kupata mafanikio.

Alisema Matarajio makubwa kwa umma ni kupata elimu iliyopo ndani ya kitabu, nachotaka kuwaambia wasomaji wanapaswa wajiandae, kitabu kina vitu vingi vipya ambavyo watu bado hawajawahi kupata kusoma au kuhadithiwa.

Utakumbuka kuwa waandishi wengi wa vitabu wamekuwa wakitazama vitu ambavyo haviwezi leta athari kubwa katika kazi zao, lakini kwa Sheikh Ponda hana woga huo, ni mtu ambaye hajawahi kurudi nyuma katika jambo analolisimamia, hivyo hata kwenye uandishi wa kitabu hiki ameandiika vitu vya kweli hata kama vinaumiza.

Watu watarajie vitu muhimu ambavyo vinaweza saidia katika historia ya harakati za waislam na jamii kwa ujumla, ndani ya nchi na nje ya nchi

Aidha kuhusu ushauri wangu kwa jamii ni kwamba niwaombe wafanye jitihada za kupata kopi ya kitabu hiki cha Juhudi na changamoto, ni kitabu ambacho hutajutia kukisoma, kimejaa mambo mazuri na hakichoshi katika usomaji wake.

Mbali na kutoa wito kwa jamii kukisoma kitabu cha Sheikh Ponda, pia amewakumbusha masheikh na viongozi wa kada mbalimbalin kujenga utamaduni wa kuandika vitabu, kwani anaamini kuwa katika uongozi watu wanajifunza mambo mengi.

“Mfano kwenye jamii ya Kiislam, watu wasingesoma historia ya uongozi wa Mtume kama hakuna waandishi, kama maisha yake yasingeandikwa basi kuna vitu vingi ambavyo umma usingejifunza,” alisema.

Vilevile alisema watu waandike chanya na hasi, hata kama ikitokezea hukufanya vizuri katika eneo lake kwa sababu kadhaa ni vizuri akaziandika na watu wakajifunza jambo hilo.

“Tunatamani kuona watu wanajifunza ili kuboresha au kuongeza katika jambo husika, uzoefu ni mwalimu mzuri, watu wasidhani kuandika ni jukumu la watu flani, hapana hili ni jukumu letu na tunapaswa kutoa elimu kwa vizazi vinavyokuja” aliongeza.

Aidha akieleza jambo ambalo limemfurahisha baada ya kukiona kitabu hiko, Mkondo alisema yapo mambo mengi yamenifurahisha lakini kubwa ni ni ukweli usio na woga ambao Sheikh Ponda ameueleza.

Alisema Watu wengi wamekuwa na tabia ya kuandika vitabu kwa kuvicha baadhi ya taarifa ama kuweka lugha za mafumbo kwa kuzingatia sababu mbalimbali jambo ambalo Sheikh Ponda hakukifanya. Sheikh amekuwa mkweli na muwazi kitu ambacho hata wasomaji wakisoma watanufaika nacho

Alisema Kitabu kina rejea za kutosha, data za kutosha, hakuna kitu cha kubabaisha na anaamini watu wakisoma watapata elimu sahihi sio vitu ambavyo vimetengenezwa tengenezwa.

Akieleza upatikanaji wa kitabu hicho, Mkondo alisema Vitabu vitapatikana nchi nzima, tayari wamejipanga kuweka mfumo mzuri ili watu wengi waweze kupata kitabu.

Sheikh Ponda Issa Ponda anatarajia kuzindua kitabu chake cha Juhudi na Changamoto, Jumapili 4, 2022 katika ukumbi wa Peacock hotel, Jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa tatu hadi kukamilika kwake saa sita

Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Dkt Omar Tego, msomi wa siku nyingi anayefanya kazi Chuo Kikuu cha Kiislam MUM

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, kitabu cha Juhudi na Changamoto kwa awamu ya kwanza wanatarajia kudurufu kopi 5,000 na kusambaza katika maduka yote ya Ibn Azim, lakini pia mikoani kutafanyika mipango ili kiwafikie kwa urahisi.

Mbali na kitabu cha Juhudi na Changamoto ambacho tayari kimeshakamilika kwa asilimia 100, Sheikh Ponda tayari amekamilisha miswada ya vitabu vingine 15 kwa asilimia 90 na vitaanza kuachiwa hatua kwa hatua.

Vitabu ambavyo tayari miswada yake imekamilika kwa asilimia 90% ni pamoja na kitabu cha Wako wapi raia hawa, Pitio la Zanzibar, Matukio na Habari, Ukweli katika utafiti wa Sivalon, Mahakama ya Kadhi Tanzania pamoja na Kiswahili Chawekwa Rehani.

Vingine ni Hijja Kongamano la Ulimwengu, Mwembechai, Mazingatio (Consideration), Masheikh gerezani, Ulamaa na Majukumu, Waislam na Mkono wa Dola, Mantiki za Ndoa za Mtume, Mafunzo ya umoja na Harakati za Vijana Sita.

 Sheikh alisema kitabu cha Juhudi na Changamoto kinapatikana kwa Shilingi 15000.


 

 

 

Hakuna maoni