Zinazobamba

Ni msimu wa ukame, wananchi fanyieni kazi maelekezo ya TMA

 



Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania TMA, Dkt Agnes Kijazi aliwasihi wadau mbalimbali  wa mamlaka hiyo kujipanga vizuri kukabiliana ukame ambao unatarajiwa katika msimu wa vuli unaoanza Oktoba hadi Disemba 2022.

Katika nasaha zile, Dkt Kijazi  alinukuliwa akisema mifumo ya hali ya hewa imeonyesha uwepo wa kipindi kirefiu cha ukavu katika maeneo mengi ya nchi, huku sekta mbalimbali zikitarajiwa kupata athari kwa ukosefu wa mvua.

Alinukuliwa akisema “Kwa ujumla mvua za vuli zitakuwa chini ya wastani hadi wastani, pia msimu unatarajiwa kuanza kwa kuchelewa na kuambatana na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,”

Akieleza mvua zitakavyokuwa, alisema kwa Kanda ya Ziwa Viktoria hasa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo na Kakonko) kutakuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na kwamba mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2022.

Pia, katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Simiyu mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2022. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2023.

Kwenye ukanda wa Pwani ya Kaskazini  hasa mikoa ya Morogoro, Pwani, visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba nako zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na mvua zake zitaanza kunyesha  kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022 na kuisha kwake Januari 2023.

Pia nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kutakuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022.

Kutokana na utabiri huo, Dkt Kijaz ametoa maelekezo kwa wadau kutumia chakula kwa uangalifu, toka ngazi ya kaya hadi taifa bila kusahau kutumia mvua chache zitakazojitokeza kwa faida.

Kwa upande wa wafugaji na wavuvi amewashauri kuhifadhi malisho kwani kuna uwezekano kutokea kwa uhaba wa upatikanaji wa maji.

Ushauri mwingine kwa wafugaji ni kuendelea kuwataka kufuatilia maelekezo yanayotolewa na maafisa ugani na kujenga tabia ya kufuatilia utabiri wa mamlaka kujua hali inavyokwenda

Pia kwenye Sekta ya utalii na wanyama pori, Dkt Kijazi alisema wanyama pori wanaweza kutoka porini kutafuta malisho sehehmu zingine kwa sababu ya kukosa malisho hifadhini na kuzishauri mamlaka kutoa elimu ili kuwakinga watu wanaozunguka maeneno yao na hatari ya kuvamiwa na wanyama

Kwenye upande wa Usafiri na usafirishaji, alisema ni muda mzuri wa kuendeleza mipango ya uboreshaji wa miundo mbinu, ujenzi unaoendelea basi ufanyike kwa kufuata utabiri wa hali ya hewa.

Nao waandishi wa habari wametakiwa kuendelea kuhabarisha umma habari sahihi kutoka mamlaka kwani kufanya hivyo kunaongeza elimu kwa umma.

“Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mwenendo wa msimu wa Vuli pamoja na taarifa zilizohuishwa za hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),” alisema

Ni matumaini yetu kuwa maelekezo yaliyotolewa na mamlaka yatafanyiwa kazi na wadau wote kuanzia wakulima, wafugaji, maafisa mipango miji, wizara husika kwa lengo la kuleta ufanisi kwenye jamii yetu.

Ends

 

Hakuna maoni