Zinazobamba

Wipahs, Tronic yagawa sadaka ya futari kwa Watu 1000, waombewa dua

 


Mmoja wa wanufaika wa sadaka ya Futari akiondoka baada ya kupewa futari yake na waratibu.




Na Selemani Magali

Taasisi isiyo ya kiserikali ya World Islamic Propagation and Humanitarian Services (WIPAHS) kwa kushirikiana na Kampuni ya usambazaji ya vifaa vya umeme vya Tronic wamefanya hafla fupi ya kutoa sadaka ya futari kwa watu wenye mahitaji maaalum wapatao 1000 kutoka katika wilaya za Temeke na Ilala dhamira ikiwa ni kuwafariji hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa zoezi hilo, Bi Amina Mubaraka amesema wamegawa futari hiyo bure kwa watu wenye matatizo ya kuona, walemavu wa viungo pamoja  na walemavu wa ngozi (albinism).

“Ni utamaduni wetu ambao tumejiwekea kufuturisha, huwa tunaangalia makundi maalum pamoja na yale ya kawaida, tulishagawa kwa makundi ya kawaida wiki iliyopita, taasisi inatamani kuwaona ndugu zetu hawa wanakuwa katika faraja na waungane na waislamu wengine katika kuendeleza ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani,” aliongeza.

Aidha Amina amesema wamegawa jumla ya vifurushi 1000 ambapo kila kifurushi kimoja kilikuwa na mchele aina ya Korie (fragrant premium) kilo 5, Sukari kilo 5 na maharage kilo 5.

Mmoja wa wanufaika wa sadaka hiyo, Bi Hadija Abdallah amewashukuru taasisi ya Wipahs pamoja na Tronic kwa moyo wao wa kujitoa na kuwafaraji kwa futari katika kipindi cha Ramadhani.

Amewaombea dua kwa Mwenyezi Mungu waendelee kuwa waadilifu na wenye moyo wa kutoa ili watu wanaostahiki waweze kupata sadaka hiyo kama ilivyokusudiwa.

Katika hatua nyingine, Taasisi hiyo imeendesha semina ya siku moja kwa walimu, ikiwa ni jitihada yao ya kuwajengea uwezo walimu ili kuwalea vijana katika malezi yanayompendeza Allah.

Amina amesema kila ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhani, taasisi hiyo huwa inatenga siku moja kwa ajili ya kuwafunda walimu juu ya dhima kubwa waliyonayo ya kuwalea vijana kimaadili.

“Semina inawahusu walimu kutoka shule za serikali na zile za watu binafsi (Private school), wanakutana na kujadiliana changamoto za malezi huko shuleni na kutafuta ufumbuzi wake,” alisema.

Aidha akielezea tija ya mafunzo hayo, Amina amesema yamekuwa yakisaidia sana kuwapa kujiamini walimu hasa linapokuja suala la kutatua changamoto katika vituo vyao vya kazi.

“Tumekutana na walimu 240, wapo walimu wa dini lakini pia wapo wasio wa dini, hawa wote watakuwa mabolozi katika shule zao, tunaamini hawatabaki kama walivyo, watakwenda kusaidia kuwalea watoto kwa mujibu wa kitabu cha Allah kinavyosema,” aliongeza

Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo, Sheikh Abutchi Saidi kutoka Wilaya ya Kibaha amesema semina hizo nimuhimu katika kuwajenga walimu kiimani.

“Nilikuwa natoa mada ya nafasi ya mwalimu katika kueneza dini, mwenzangu alikuwa anatoa mada ya Imani ya mwalim katika jamii, ukiziangalia mada hizo zote zinalenga kumkumbusha mwalimu juu ya imaani,” alisema

Walimu hawajui kuwa ualimu wake unaweza kuwa chachu ya watu kupenda dini yake, mwalimu ni kioo cha jamii, watu wanaweza kufikia mahala wakabadilisha dini zao kwa kuona mazuri yanayofanywa na mwalimu

Naye Khadija Litunu Hamadi, Mwalim wa shule ya msingi Kingugi na mhitimu wa shahada ya kwanza ya ualimu kutoka chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro amezishauri taasisi zingine ziige mfano huo kwani mafunzo hayo ni muhimu.

Amesema mafunzo hayo ni chachu ya kubadilika kiiutendaji kwa walimu kwani yanahamasisha kuwa na busara katika kazi ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika vituo vya kazi ukizingatia kuwa wanahudumia watu wengi wenye tabia tofauti.



Hakuna maoni