Zinazobamba

Wakurugenzi waagizwa kufufua Madarasa ya MEMKWA, kutenga fedha za walimu




Serikali imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafufua madarasa ya Elimu ya Watu ya Wazima (MEMKWA) pamoja na kutenga fedha za kuwalipa walimu wanaofundisha madarasa hayo lengo likiwa kuendelea kupunguza kundi la watu wasio jua kusoma na kuandika pamoja na kuwaongezea ujuzi unaoendana na mazingira yao.


Aidha, imewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote kufanya kampeni ya kutoa hamasa itakatayosaidia watu kujitokeza kupatiwa elimu katika maeneo yaliyotengwa kutolea elimu hiyo.

Maagizo hayo yametolewa jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Shule Kuu ya Elimu ya chuo hicho.

Amesema kuwa kuna maeneo ambayo madarasa ya kutolea elimu yamekufa hivyo na juhudi za dhati zinatakiwa kufanywa na wakaurugenzi kuyarudisha na kuwahimiza watu waliokosa fursa ya kupata elimu kuhudhuria.

" Wakurugenzi wote wayafufue madarasa ya MEMKWA katika maeneo ambayo hakuna vile watenge fedha za kulipa walimu tunafanya kuendeleza juhudi kupunguza ujinga wa kutojua kusoma na kuandika," amesema Majaliwa.

Ameiagiza Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na UDSM kufanya tafiti kuhusu takwimu halisi za idadi ya watu waliofaidika na elimu hiyo, wasionufaika pamoja na kuja na njia za kukabiliana na changamoto zinazoikabili elimu hiyo.

Maagizo mengine ni Wizara ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia kusimamia misingi ya kuanzishwa taasisi hiyo kwa kuhkikisha inapunguza idadi ya watu wajinga,taasisi ya elimu hiyo kuandaa mkakati wa kuifikisha maeneo ya vijijini sio mijini tu, kuimarisha mfumo thabiti kwa wanakisomo kwa kila mwaka kwa kuimarisha programu, mitihani na utoaji vyeti kwa wahitimu.

Waziri wa wizara hiyo Profesa Joyce Ndalichako amesema maadhimisho yanafanyika kuendeleza mchango wa elimu hiyo kwa taifa tanngu ilipotangazwa mwaka 1970.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo amesema utaoji wa elimu hiyo ni mwendelezo wa kutekeleza lengo la nne ya Malengo ya Millenia ya kuhakikisha jamii inapata elimu jumuishi.

Kwa upande wake Amidi Mkuu wa Shule hiyo Daktari Kafanabo amesema kongamano hilo linaenzi mchango Hayati Mwalimu Julius Nyerere katika kuikomboa nchi katika maradhi ya ujinga, umaskini na maradhi kupitia elimu hiyo.
 
Dkt. Kafanabo amesema kongamano litaangalia wapi elimu hiyo ilipotoka na inapokwenda na kusisitiza kuwa mawasilisho mbalimbali yatatolewa na watalaam wa taasisi mbalimbali.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William Anangisye amesema uhai wa chuo upo kwenye tafiti na kwamba kongamano hilo limeandaliwa ili kufanya tathmini ya elimu hiyo ilipofikia na inapoelekea.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori amesema  amempongeza waziri Majaliwa na kusema kongamano hilo litaibua mawazo yatakayosaidia kukabiliana na ujinga.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Michael Mumbi amesema kazi yao ni kusanifu vijana na watu wazima  wasio jua kusoma na kuandika kupata ustadi na kuwaondolea ujinga.

Katika kongamano hilo Tuzo za Shahada za Umahiri katika Mchango wa kuendeleza elimu hiyo zilitolewa ikiwemo ya Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika kupinga ujinga kupitia elimu hiyo.

Hakuna maoni