Zinazobamba

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAGAWA HATI ZA UMILIKI ARDHI MKOANI MBEYA

 


Kamishna wa Ardhi Msaidi Mkoa wa Mbeya Bi. Syabumi Mwaipopo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kabla ya kwenda uwandani kukagua miradi hiyo

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula akitoa elimu kwa wananchi wa Mtaa wa Ituha (hawapo kwenye picha) kuhusu faida ya Kupanga, Kupima na Kumilikishwa maeneo yao wakati Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipotembelea Mtaa huo kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi

Wajumbe wa Kamti ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa Miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi Mkoani Mbeya iliyosomwa na Kamisha wa Ardhi Msaidizi Mkoa

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakikagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi eneo la Iziwa- Mbeya Peack baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji ya mradi huo

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakiongozwa na Mhe. Angelina Mabula (mwenye miwani) Naibu Waziri Wizara ya Ardhi wakikagua ramani ya upimaji ya mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Mbeya Peack

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Ituha wakifuatilia taarifa ya mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi kwenye Kata hiyo ikiwasilishwa mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii (haipo kwenye picha) wakati wa ukaguzi na ugawaji hatimiliki kwenye mradi huo

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Ituha, wakifurahia hatimiliki zao walizokabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Aloyce A. Kwezi wakati kamati hiyo ilipoenda kukagua utekelezaji wa mradi wa Kupanga, Kupima na Kumiliksha ardhi eneo la Ituha


Na Eliafile Solla

 Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imefurahishwa na utekelezaji wa miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi Mkoani Mbeya ambapo baadhi yake imekamilika na mingine inaendelea baada ya kupokea taarifa za miradi hiyo, kuikagua na kisha kugawa hatimiliki kwa baadhi ya wananchi walionufaika na miradi hiyo.

 

Taarifa hiyo ya utekelezaji miradi na kazi za sekta ya ardhi imesomwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa Bi. Syabumi G. Mwaipopo ambapo aliweka bayana kwamba katika mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ilitoa mkopo wa fedha kiasi cha Tsh. 639,973,000/= kwa Halmashauri ya Jiji ili zitumike Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.

 

Mwaipopo alisisitiza kwamba, wataalam wa sekta ya ardhi walifanya utafiti ili kujua ni eneo gani mradi ungetekelezwa na baadae eneo la Iziwa – Mbeya Peack lilitwaliwa kwa ajili ya mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi na ulihusisha kazi mbalimbali kama vile utwaaji ardhi, kufanya uthamini na kulipa fidia pamoja na kuchonga barabara.

 

‘‘Katika mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi eneo la Mbeya Peak, lengo lilikuwa kupima viwanja 600 lakini viwanja vilivyopatikana baada ya upimaji vilikuwa 564, na kati ya hivyo viwanja 515 tayari vilishauzwa’’, alisema Mwaipopo

 

Aliongeza kwamba, baada ya mradi wa Mbeya Peak, mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ilitoa tena fedha kiasi cha Tsh. 30,000,000 ambazo zimetumika kutekeleza mradi mwingine wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha katika Mtaa wa Ituha, mradi ambao umefanikiwa kwa kiasi kikubwa na hatimilki zimeshaanza kutolewa tayari kwa viwanja vyote ambavyo upimaji wake umekamilika na malipo kufanyika.

 

Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mbeya katika mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Ituha ilikusudia kupima viwanja 500 lakini hadi sasa jumla ya viwanja 706 vimepimwa na viwanja 34 tuu ndivyo vilivyomilikishwa tayari kwa maana ya hatimiliki zilizokamilika.

 

Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi na kazi za sekta ya ardhi Mkoani Mbeya Mhe. Jafary Wambura Chege, mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii alisema, Jiji la Mbeya ambako ndiko anakotoka Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limeonesha mfano mzuri sana katika kutekeleza miradi hasa ya Upangaji, Upimaji na Umilikishaji ardhi ukilinganisha na Mikoa mingine walikopita hadi sasa.

 

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Aloyce A. Kwezi aligawa jumla ya Hatimiliki kumi (10) kwa baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Ituha baada ya zoezi zima la Kupanga na Kupima maeneo yao kupitia mradi kukamilika kama njia ya kuwahamasisha wananchi ambao bado hawajalipia gharama za umilikishaji katika mtaa huo wa Ituha.



Hakuna maoni