Wiki ya magonjwa yasiyoambukiza yazinduliwa, Wataalamu wizara ya afya wataka wananchi kuwekeza kwenye afya
Imeelezwa kwamba magonjwa
yasioambukizwa yameendelea kuitikisa Tanzania ambako imefikia hatua katika kila
kundi la watu wanne mtu mmoja ana maradhi hayo huku vifo navyo vikiwa juu
ambapo katika kila vifo 3 vinavyotokea mmoja wao anakufa kwa magonjwa hayohayo.
Akizungumza na mwandishi wa Tizii
Media, Meneja mpango wa mpango wa taifa wa kuzuia na kuzibiti magonjwa
yasiyoambukiza kutoka Wizara ya afya (NCD), Dkt Omari Mbuyu alisema hali
imezidi kuwa mbaya na kuwataka watanzania kuwekeza katika afya zao ili kuzibiti
maradhi hayo.
“Suala la afya ni jukumu letu, Wizara
inakauli mbiu kuwa afya yangu mtaji wangu kwa hiyo lazima tuwekeze katika afya
zetu, ukifanya mazoezi, ukiacha sigara, ukiacha pombe, ukizingatia mlo kamili
maana yake unawekeza katika afya yako, kama taifa tujitahidi kuwekeza katika
afya zetu,” alisema Dkt Omari.
Aliongeza kusema takwimu za hivi
karibuni (2016) zinaonyesha kuwa kwenye kundi la watu wanne mmoja anashinikizo
la damu, katika watu 10, mmoja anatatizo la kisukari, katika kila vifo vitatu
basi mtu mmoja anakufa kwa ugonjwa usioambukizwa.
“Tupo hapa leo kuazimisha wiki ya magonjwa
yasioambukiza, lengo kuu ni kujenga uelewa na hamasa juu ya magonjwa
yasiyoambukiza kwa wananchi, kama taifa bado tuna hali mbaya, nguvu kubwa
inahitajika ili kuiamsha jamii kupambana na maradhi haya,” aliongeza Dkt Omari.
Alitaja mfano wa magonjwa
yasioambukizwa kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari, saratani, magonjwa
ya akili, baadhi ya magonjwa ya afya ya kinywa na meno, saratani za macho na
mengine mengi ambayo yanaweza kuzuilika kama tutawekeza muda wetu na fikra zetu
huko.
“Magonjwa karibu yote yanasabababishwa
na vitu vinne, navyo ni ulaji wa hovyo, matumizi ya pombe kupita kiasi, matumizi
ya sigara ya kiwango chochote kile pamoja na kutofanya mazoezi, kama tunahitaji
kubaki salama lazima tuchunge afya yetu kwa kufanya mazoezi, kula kwa
mpangilio, kuacha pombe na sigara.
“Kwa wastani mtu mzima anatakiwa
kufanya mazoezi kwa dakika 30, sawa na dakika 150 kwa wiki, na ni mazoezi
yoyote yale ambayo yataweza kukutoa jasho, au shughuli ya kijamii, wananchi
fanyeni jitihada katika hilo,” aliongeza.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam
Mhe. Aboubakar Kunenge amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanafanya mazoezi na
kuepuka ulaji usiofaa ili kujikinga na magonjwa yasiyo ambukizwa.
Aidha Kunenge amesema kwakuwa magonjwa yasiyo
ambukizwa yanaweza kuzuilika ni vyema wananchi wakaanza kuchukuwa tahadhari
mapema kwa kuhakikisha wanazingatia ulaji Bora, kupunguza ulevi usiofaa, kupunguza
uvutaji wa sigara na kuzingatia michezo.
Pamoja na hayo RC Kunenge amesema
Upande wa Serikali itaendelea kutoa elimu ya kutosha ya namna Bora ya
kukabiliana na magonjwa hayo na kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu
mbalimbali ya Afya
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wamefanya Ufunguzi wa wiki ya kitaifa ya kukabiliana na
Magonjwa yasiyoambukiza iliyoanza November 07 2020 na kufikia kikomo chake
Novemba 14, 2020, katika wiki hiyo matukio mbalimbali yatafanyika ikiwamo
michezo ya mpira wa miguu, kuendesha baiskeli, mpira wa mikono, mbio na michezo
mingine mingi. Mbali na michezo pia wananchi watapata fursa ya kupima magonjwa
mbalimbali bure na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni