Kongamano la pili la magonjwa yasioambukiza lafanyika dar, watafiti Tanzania watakiwa kufanya tafiti za dawa asili
Washiriki wa Kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi |
Mkurugenzi wa idara ya tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Grace Maghembe na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia ufunguzi wa kongamano hilo ambalo litakua la siku mbili |
Na Mwandishi wetu
Kufuatia ongezeko la matumizi ya dawa asili hapa Tanzania hasa
wakati ule wa janga la Corona (covid-19), serikali imetoa wito kwa watafiti
kufanya tafiti ili kutoa majawabu sahihi juu ya uwezo wa wa dawa hizo juu ya
kukabiliana na magonjwa yasioambukiza.
Hali ilivyo katika jamii, wananchi wengi wanatumia dawa asili
zikiwemo za shinikizo la damu, kisukari, saratani lakini bado hakuna tafiti
ambazo zimefanywa kuonyesha kuwa dawa hizo zinatibu kwa asilimia inayotakiwa.
Hayo yamebainishwa na Mganga
mkuu wa serikali, Prof Abel Makubi katika kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza
lililofanyika katika ukumbi wa JNICC, jijini Dar es Salaam.
“Tunahitaji tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali
za afya, wakati wa mlipuko wa Covid-19 wengi tulirudi kwenye dawa zetu za asili
muda umefika sasa tupate majibu ya kisayansi yatakayotuonesha kwenye zile dawa
kulikuwa na kemikali gani.
“Aidha tunatambua kuna dawa nyingi sana za asili zinatumika
kutibu pumu, shinikizo la juu la damu, saratani na mengineyo hivyo
tunawakumbusha watafiti na taasisi zetu zote za utafiti kufanya tafiti za dawa
hizi ili wananchi wetu wapatiwe taarifa sahihi za dawa hizi,”ameeleza Prof
Makubi.
Amesema mchango wa tafiti mbalimbali ni muhimu iwapo utazingatia
zaidi ubunifu, ugunduzi wa dawa na chanjo mbalimbali zitakazosaidia kupunguza
magonjwa na vifo vinavyozuilika.
Magonjwa yasiyoambukiza (Non-Communicable Diseases) yanaendelea
kuongezeka nchini ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa mwaka 2017 sawa na
asilimia 33 ya vifo vyote.
Prof Makubi aliongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yamesababisha
hasara kubwa kwa maana ya kuondoa nguvu kazi na kurudisha nyuma maendeleo ya
mtu binafsi na taifa kwa ujumla na hivyo kusababisha utegemezi sugu kwa familia na pia
kuongeza mzigo mkubwa kwenye mfumo wa
afya kwa kuwa ni magonjwa yanayochukua muda mrefu na yanatumia raslimali
nyingi.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa
magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41 ambayo ni sawa na
asilimia 71 vya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
Vifo vinavyotokea nchini vinatokana zaidi na magonjwa ya moyo na
shikizo la Damu kwa asilimia 13, kisukari asilimia mbili, saratani asilimia
saba na ajali asilimia 11 hali hii kwa ujumla haikubaliki na inatufanya
tujumuike katika kujitathimini na kupanga mikakati ya pamoja.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni