Zinazobamba

NONDO ATOA MAPENDEKEZO KWA BUNGE


NA MWANDISHI WETU

  

MWENYEKITI wa Ngome ya Vijana ya Chama Cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema ili kukomesha vitendo vya utekaji ni vema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likafanya mabadiliko ya sheria kwa Askari wa Jeshi la Polisi, kuvaa sare anapokwenda kumkamata mtuhumiwa ili kuondoa taharuki.

 Ameongeza kuwa tofauti na hilo pia askari ni vema sheria nayo ikasema kwamba anatakiwa ajitambulishe na kueleza kosa la mtuhumiwa kabla ya kumkamata na aeleze anampeleka kituo gani cha Polisi ili kuwapa urahisi ndugu, jamaa kuweza kumfuatilia.

Nondo amezungumza hayo leo, Januari 9, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mazingira ya kutekwa kwake na hofu aliyonayo baada ya kuvunja masharti aliyopewa  na waliomteka wakati wakimwachia, akiamini kwamba wanaweza kumteka tena na pengine kumuua.

“Mwaka 2023, Bunge lilifanya mabadiliko na kupitisha sheria kwa mtuhumiwa kuweza kukamatwa na askari asiyevaa sare, jambo ambalo kwa sasa inaonekana kutumika vibaya, hivyo nadhani huu ndio muda wa kuifanyia mabadiliko tena ili iseme askari anapokwenda kumkamata mtu ni lazima avae sare na ajitambulishe na aseme anampeleka kituo gani,” amesema.

Nondo amesema kwamba vitendo vya utekaji vinavyoonekana kuanza kushika kasi visifumbiwe macho, kwani vinachafua sura ya nchi na kusisitiza uchunguzi ufanyike kwa matukio ambayo yameripotiwa na taarifa za uchunguzi zitolewe na isifanywe dhiaka.

Ameongeza kuwa kama havitadhibitiwa mapema vinaweza kuonekana siku zijazo kama utamaduni na inaweza kusababisha makundi ya kiharifu kuchukua mwanya huo kutimiza malengo yao na kuja kuyadhibiti inaweza kuwa ni kazi kubwa na kusisitiza muda bado hupo ya kufanyia kazi kwani amani ikivurugika haitoangalia chama ama mtu.

HOFU YA KUTEKWA TENA

Aidha ameongeza kuwa ni jukumu la kila mmoja kupaza sauti ya kulinda amani, Nondo ameongeza kuwa kwa sasa anaishi kwa hofu ya kutekwa tena baada ya kuvunja masharti yote ambayo amepewa na watu waliomteka Desemba Mosi, mwaka jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Nondo, alitekwa na watu hao wasiojulikana muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi akitokea mkoani Kigoma na kutelekezwa kwenye ufukwe wa Coco akiwa na hali mbaya na akasaidiwa na waendesha bodaboda kufikishwa katika ofisi za chama hicho Magomeni, Dar es Salaam.

Nondo ameeleza kwamba wakati anaachiwa na watekaji hao, walimtaka atekeleze masharti kadhaa yatakayomfanya kuwa huru na hasitekwe tena siku sijazo, ambayo anadai tayari ameshayavunja yote hali inayosababisha kuwa na hofu ya kutekwa kwa mara nyingine na pengine kuuawa.

“Wakati wananiachia waliambia nisiongee na vyombo vya habari jambo ambalo tayari nimelivunja, pili waliniambia baada ya pale niende nyumbani jambo ambalo nimefanya kinyume nao, tatu waliniambia nifunge mdomo nalo sijatekeleza, naaminmi wanaweza kufanya chochote hivyo suala la ulinzi wangu liko juu yangu na siwezi kutembea na walinzi ila chama kinanilinda, Mungu ananilinda,” amesema.

Ameongeza kuwa, hawezi kukaa kimya kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Ngome ya Vijana, hivyo anawajibika kusema na hatojificha, ikitokea ametekwa tena ama kuuawa itakuwa wamemtanguliza tu kwa maana kila mwanadamu atapitia kifo.

Amesisitiza kwamba hao watekaji wanaweza kumteka yeyote, hivyo wasipodhibitiwa siku za usoni yanaweza kuonekana ya kawaida hali itakayoweza kusababisha amani ambayo ni tunu ya taifa ikatoweka na kuirejesha ikawa ni kazi ngumu.


Pia ametolea mfano taifa la Mali, akidai kwamba kwa sasa liko katika wakati mgumu kudhibiti vitendo vya utekaji ambavyo vilianza kama mchezo na kusababisha makundi ya kigaidi kuingia na sasa wanateka wageni na kuomba fedha ili wawaachie.


“Kwanza Tanzania, sipendi nchi yangu ifikie huko, kazi kubwa imefanyika kuifanya nchi kuwa tulivu na kusababisha watalii kumiminika kwa wingi na pato la taifa kuongezeka, hivyo wananchi tupaze sauti kudhibiti hali hii kwa maslahi ya taifa,” amesema.

 

Hakuna maoni