Zinazobamba

Ilala Islamic yafanya mahafali ya kidato cha sita, Sheikh Alhadi Mussa awa mgeni rasmi



Issack Tadheo, Dsm

Shule ya Ilala Islamic imeshika nafasi ya tatu katika mitihani ya Mock ya Kidato cha Sita kwa wanafunzi wa Mkoa wa Dar es Salaam. 

 

Aidha shule hiyo imebainisha kuwa Julai 17 mwaka huu itafanya harambee kwa ajili ya kuchangia hosteli zilizopatwa na janga la moto. 

 

Hayo yamebainishwa jijini humo na Mkuu wa shule hiyo Buhelo Issa katika Mahafali ya Kidato cha Sita.

 

Alisema katika mahafali hayo wanafunzi 124 wamehitimu kidato hicho na kwamba kati yao wavulana ni 74 na wasichana 50 na kusisitiza kuwa matokeo hayo yamepatikana kutokana juhudi za walimu pamoja na wanafunzi kutilia mkazo masomo.

 

"Ndugu mgeni rasmi tumepata mafanikio haya sababu ya walimu kutimiza majukumu yao hata wanafunzi wanafuatilia wanachofundishwa," alisema Issa.

 

Buhelo alisema katika mitihani hiyo nafasi ya Kwanza ilichukuliwa na Shule ya Sekondari ya Fedha Wasichana, ya pili Shule ya Sekondari ya Kanosa, ya tatu wakipata wao na ya nne ikienda kwa Shule ya Sekondari ya Fedha Wavulana.

 

Aliongeza kuwa Julai 8 mwaka huu Shule hiyo ilipatwa na janga la moto na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu wa kidato cha kwanza na kuharibu vifaa.

 

Alisisitiza kuwa wanaamini kupitia mbunge wa Jimbo hilo na mkuu wa wilaya ya Ilala watapata fedha za kugharamia janga hilo.

 

Pia alisema Shule hiyo inakabiliwa na changamoto za uhaba wa wanafunzi, ucheleweshaji wa ada na kumwomba sheikh Mkuu kuwasaidia kuzitatua.

 

Kwa upande wake Sheikh Mkuu wa mkoa huo Alhad Mussa Salum aliipongeza Shule na kuipa pole kwa janga huku akiwahimiza walimu kuzingatia maadili yao ili waendelee kupata matokeo mazuri.

 

Naye mhitimu Aisha Salum alisema walipokuwa shuleni hapo walipatiwa malezi mazuri ya kiroho pamoja na masomo kwa vitendo.

 


Hakuna maoni