Zinazobamba

Familia tatu zataka vyombo vya haki viboreshwe, mahabusu wapone

 


Na Mwandishi wetu

Familia tatu za Kiislam Mkoani Mtwara zimeomba Serikali ya Tanzania Kuboresha utendaji wa vyombo vyenye dhamana ya kutoa haki ili kuondoa changamoto ya watuhumiwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu kwa madai ya upelelezi wa makosa kutokamilika

Wakizungumza na vyombo vya habari katikati ya wiki hii, familia ya wahanga ambao wako mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili sasa kwa tuhuma za ugaidi, wameeleza kusikitishwa kwao kwa haki ya ndugu zao kucheleweshwa.

Akizungumza kwa niaba ya familia hizo tatu, Tiba Moshi Athumani Kakoso alisema wameamua kupaza sauti ili vyombo vyenye dhamana visikie kilio chao kwani vijana wanaoshikiliwa ni nguzo, wameacha wazee, watoto na wake wanaowategemea kwa kila kitu.

Hivi sasa familia walizoziacha zinapita katika wakati mgumu wa kimaisha hasa mzee Mkaliaganda ambae ni mlemavu wa macho, mtoto wake Bw. Waziri Salum ndiye aliyekuwa anamsaidia kwa kila kitu kutokana na kazi yake ya ujenzi.

Sisi mnavyotuona hapa ni wawakilishi wa familia tatu, familia ya Moshi Athumani Kakoso, familia ya Salum Omar Bumbo na familia ya Suleiman Mkaliaganda ya Mtwara,

Tumewaita hapa kueleza kilio, masikitiko na sononeko letu kutokana na masahibu ya ndugu zetu ambao ni Omar Salum Bumbo (51),Ustadhi Ramadhani Moshi Kakoso (41) na Waziri Salum Sulleiman Mkaliaganda (33),

Hawa ni mahabusu katika gereza la Lilungu mkoani Mtwara, wapo hapo kwa miaka miwili sasa na wasijue hatma yao,

Watu hao walikamatwa katika nyakati tofauti mwaka 2017, kwa tuhuma za makosa ya kigaidi katika mahakama ya wilaya ya Mtwara.

Tiba Kakoso aliiomba mamlaka husika kukamilisha taratibu za kisheria ili watuhumiwa hao na wengine waliopo mahabusu, mashauri yao yatolewe uamuzi, ili kama wanahatia wafungwe na kama hawana hatia basi waachiwe huru

“Tunaiomba serikali ya wanyonge inayosimamia haki, watekelezewe kwa haraka taratibu za kisheria ili ndugu zetu na mahabusu wengine mfano wao ambao wanaendelea kukaa mahabusu kwa miaka kadhaa sasa uamuzi utolewe,

Tunaiomba serikali kesi za mahabusu wa aina hii zisikilizwe na kama ushahidi haujakamilika basi wapatiwe dhamana na kama ushahidi haupo kabisa basi waachiwe huru kuliko kubaki katika hali ya sasa ambayo inatoa sura ya wazi ya uonevu

Akielezea hatua ambazo familia imechukua kabla ya kuamua kuzungumza na waandishi wa habari ili kupaza sauti zao, Tiba Kakoso alisema suala la mahabusu hao ameshalifikisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP), ambao nao walikili kupokea faili la watuhumiwa hao na kuahidi kulifanyia kazi.

“Kabla ya kuzungumza na nyie waandishi wa habari tulifanya jitihada nyingi ikiwamo kwenda Dodoma katika ofisi ya DPP, taarifa ni kwamba yeye alisema mafaili ya ndugu zetu hawa watatu yapo ofisini kwake na kwamba atayashughulikia,” alisema.

Akihadithia mazingira ya kukamatwa kwao, Tiba Kakoso alisema mnamo Octoba 27, 2017 Omar Salum Bumbo aliyekuwa anaishi Tandika Relini, Dar es salaam, fundi mjenzi alinyakuliwa na kutekwa na wanaoaminika kuwa ni maafisa wa usalama, aliwekewa mtego na maafisa hao kuwa wanataka kumpa kazi ya ujenzi huko Tabata na alipofika eneno la tukio ili apewe hiyo kazi ya ujenzi akaishia kutiwa nguvuni, baada ya siku tatu kupita naye mwalimu wa dini ya kiislamu na mfanya biashara, Ustadhi Ramadhani Moshi Kakoso alitiwa nguvuni nyumbani kwake Magomeni Makuti, Jijini Dar es salaam.

Aliendelea kusema kuwa baada ya wawili hao kutiwa nguvuni walipelekwa Mtwara na kuunganishwa na mtuhumiwa mwingine wa tatu Bw. Waziri Suleiman Mkaliaganda, mwalimu wa sekondari Mtwara mjini.

Alisema walifikishwa mahakamani Desemba 5, 2017, tokea hapo kesi yao imekuwa ikitajwatajwa tu, mpaka sasa bado haijaanza kusikilizwa kutokana na ushahidi kutokamilika.


Hakuna maoni